Sports Leo

Dodoma Jiji Fc Yamkomalia Straika Huyu

Uongozi wa klabu ya Dodoma Jiji Fc uko katika mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Paul Peter, baada ya alionao sasa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu.

Mabosi wa klabu hiyo wanaona bado wana uhitaji na mshambuliaji huyo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu na kombe la Shirikisho la Crdb nchini.

Hayo yamethibitishwa na mshambuliaji huyo aliyesema kuwa ni kweli yupo katika majadiliano ya kusaini mkataba mpya na kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati yake na uongozi wa timu hiyo.

“Mkataba wangu unaisha msimu huu na tayari mazungumzo ya kuongeza mwingine yanaendelea, uliopo mezani ni wa miaka miwili zaidi wa kuendelea kuichezea Dodoma Jiji, ingawa suala la kubaki au kuondoka kwa sasa ni asilimia 50 kwa 50,” alisema nyota huyo wa zamani wa Azam Fc.

Hata hivyo klabu hiyo itakutana na ushindani mkali kutoka kwa timu nyingine zinazohitaji saini yake, ingawa ameweka wazi kipaumbele cha kwanza ni sehemu anayoitumikia kwa sasa msimu huu.

Taarifa zinaeleza, Al Dahra Tripoli FC ya Libya bado inamuhitaji mshambuliaji huyo kwa ajili ya kuongeza nguvu, baada ya ofa ya kwanza waliyoiwasilisha Januari 2025, kugonga mwamba kwa kile kilichoelezwa waliwasilisha kiasi kidogo cha fedha.

Nyota huyo wa zamani aliyekulia akademi ya Azam Fc kisha kupandishwa timu ya wakubwa, akiichezea pia KMC na Tanzania Prisons, amefunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara na kuasisti mawili kati ya 30, yaliyofungwa na kikosi hicho msimu huu.

Exit mobile version