Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Injinia Hersi Said amesema kiungo wa Simba Ibrahim Ajibu sio miongoni mwa wachezaji watakaovaa uzi wa Yanga msimu ujao.
Siku za karibuni kuliibuka tetesi zilizomuhusisha Ajibu kusajiliwa na Yanga. Ni tetesi zilizoibua makundi miongoni mwa mashabiki wa Yanga wengine wakipinga usajili huo huku wengine wakiunga mkono.
Injinia Hersi amesema Ajibu sio miongoni mwa wachezaji walio katika mpango wa usajili wa mabingwa hao wa kihistoria.
Aidha amedokeza kuwa tayari wamekamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji ambao watatambulishwa wakati mwafaka ukifika
Hakuna shaka miongoni mwa wachezaji hao ni mlinzi wa kulia Djuma Shaban anayetua kutoka klabu ya AS Vita huku akisema kutakuwa na utaratibu tofauti wa kutambulisha wachezaji wapya
“Ndio tutakuwa na utaratibu wa utambulisho wa wachezaji wapya, tutawaeleza kupitia vyombo vyetu rasmi, sio yeye tu (Djuma) ila na wengine ambao tutakuwa tumemalizana nao,” Injinia Hersi aliiambia Clouds Fm