Je Yanga Sc Ipo Tayari Kupambana na Vigogo Kama Al Ahly Caf?

by Dennis Msotwa
0 comments

Baada ya droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufanyika, macho ya Watanzania sasa yanaitazama Yanga SC, bingwa mtetezi wa Tanzania Bara, ambaye amewekwa Kundi B lenye miamba mikubwa ya soka barani  Al Ahly ya Misri, FAR Rabat ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria. Swali kubwa ambalo linaendelea kuwasha moto miongoni mwa mashabiki ni moja tu: Je, Yanga ipo tayari kupambana na kufuzu robo fainali mbele ya vigogo hawa?

UBORA WA YANGA KWA SASA

Kwa kuangalia takwimu za msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ipo katika hali nzuri ya ndani. Wakiwa kileleni mwa msimamo baada ya mechi nne, wakishinda tatu na kutoa sare moja, wamefunga mabao tisa na kuruhusu bao moja pekee  ishara kuwa bado wana uimara fulani wa kiuchezaji na nidhamu ya kiufundi. Hata hivyo, tofauti kubwa ya msimu huu ni mabadiliko ya benchi la ufundi ya mara kwa mara yaliyotokea klabuni hapo kuanzia msimu uliopita kutoka kwa Miguel Gamondi kuja Sead Ramovic mpaka Miloud Hamd huku sasa kocha mpya, Pedro Gonçalves, amechukua mikoba kutoka kwa  Roman Folz, na bado anatafuta mfumo unaoendana na falsafa yake.

Je Yanga Sc Ipo Tayari Kupambana na Vigogo Kama Al Ahly Caf?

Wakati Yanga sc chini ya Nabi Yanga ilikuwa timu yenye kasi, ubunifu na uelewano mkubwa hasa kupitia wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Khalid Aucho na Fiston Mayele, kikosi cha sasa kimepoteza sehemu ya utulivu huo ambapo Chini ya Miguel Gamondi ilimpoteza Mayele pekee na ikawa na ubora ule ule lakini sasa imewapoteza karibia wote hao akiwemo Aziz Ki,Chama,Khalid Aucho na n.k.

banner

Wachezaji wapya kama Balla Conte, Lassine Kouma, Andy Boyeli na Celestine Ecua bado hawajapata muunganiko wa kutosha na wakipambana na mabadiliko ya kimazingira. Wakati mwingine wanacheza kwa vipindi, wakionesha vipaji binafsi lakini si “chemistry” ya kikosi kinachotaka kushindana na mabingwa wa Afrika kama Al Ahly.

KIWANGO CHA WAPINZANI WAO

Kwa upande wa Al Ahly, licha ya kuwa nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Misri wakiwa na pointi 23 baada ya michezo 12, timu hiyo bado inabaki kuwa tishio kubwa Afrika. Ni klabu yenye uzoefu mkubwa zaidi katika michuano hii, ikiwa na mataji 11 ya CAF Champions League. Ingawa wamebadili kocha kutoka Jose Riveiro kwenda kwa Jess Thorup wa Denmark, mfumo wao wa ushindani na wachezaji waliokomaa kama Emam Ashour,Ahmed Sayed,Achraf Bencharki bado unawapa faida kubwa.

Je Yanga Sc Ipo Tayari Kupambana na Vigogo Kama Al Ahly Caf?-www.sportsleo.co.tz

Al Ahly hawahitaji muda mwingi kuingia kwenye kasi ya kimataifa huku wakitoka kucheza michuano mikubwa ya Inter-club ambayo imezidi kuwaimarisha zaidi,ni timu ambayo haina huruma inapocheza na wapinzani wasiokuwa na uzoefu wa kutosha.

Timu ya FAR Rabat ya Morocco nayo ni ya kuogopwa. Mpaka sasa hawajapoteza mechi yoyote kwenye ligi ya Morocco, wakishinda michezo mitano na kutoka sare mitatu. Ulinzi wao ni imara, wakiruhusu mabao machache mno (wamefungwa mara chache tu katika michezo minane). Morocco kwa sasa ni taifa linalokua haraka kisoka, na timu kama FAR zimejijengea nidhamu ya mchezo wa kiufundi na kasi ya kuvutia.

Kwa upande wa JS Kabylie ya Algeria, ingawa kwa sasa wanashika nafasi ya saba kwenye ligi yao ya ndani wakiwa na alama 15, hawawezi kubezwa. Ni timu yenye historia kubwa ya michuano ya CAF, na inapocheza nyumbani nchini Algeria, mazingira ya baridi na presha ya mashabiki huwa changamoto kubwa kwa timu za Afrika Mashariki kama Yanga.

NAFASI YA YANGA KUJIPENYA

Kihalisi, Yanga ina nafasi ya kufuzu robo fainali, lakini ni ndogo kama mambo hayatabadilika haraka. Kwanza, wanahitaji kujenga muunganiko wa wachezaji wapya na wa zamani, jambo ambalo litahitaji muda na nidhamu ya mazoezi makali. Pili, mchezo wa ugenini utakuwa kipimo halisi. Ili kuendelea mbele, Yanga italazimika kupata angalau ushindi wa nyumbani katika michezo yote mitatu, na kuvuta angalau pointi moja au mbili ugenini — jambo linalohitaji uimara wa kisaikolojia na kiufundi.

Kipimo kingine ni ubora wa benchi la ufundi. Kocha Pedro Gonçalves ana uzoefu wa soka la Afrika akiwa amewahi kufanya kazi Angola, lakini CAF Champions League ni ngazi nyingine yenye presha kubwa. Hivyo, mbinu zake na ushawishi wake wa kisaikolojia vitakuwa muhimu sana kuamsha morali ya wachezaji wapya.

HITIMISHO

Kwa sasa, Yanga inabaki kuwa timu yenye roho ya ushindani, lakini si timu iliyokamilika kupambana na wakongwe wa Afrika. Ukosefu wa mastaa kama Aziz Ki, Aucho na Chama na Kennedy Musonda ni pigo kubwa, na hadi sasa safu mpya haijaonyesha ubora wa kuaminika katika mechi kubwa. Hata hivyo, kama watafanikiwa kujenga umoja wa timu, kutumia faida ya mechi za nyumbani pale New Amaan Complex, na kocha Gonçalves akipata mfumo thabiti mapema, basi Yanga inaweza kuwashangaza wengi na kuibuka moja ya timu zitakazovunja rekodi kwa kufuzu robo fainali.

Lakini kwa sasa  kwa mtazamo wa kiufundi na takwimu  Yanga ipo njiani, bado haijafika. Mfumo upo, morali ipo, lakini ubora wa uchezaji na muunganiko wa kikosi ndio kitakachoamua kama “Wananchi” watapita salama au watajikuta wakibaki na historia tu ya kufika hatua ya makundi.

You may also like

Leave a Comment

Enable Notifications OK No thanks