Mashabiki wa Simba SC wameshaanza kushtuka mapema baada ya taarifa mpya kutua rasmi kwamba jezi za msimu mpya sasa zitazinduliwa Jumapili ya tarehe 31 Agosti 2025 badala ya tarehe ya awali iliyokuwa Agosti 28. Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika kwa ubora wa hali ya juu katika ukumbi wa kifahari wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam. Hili ni tukio linalosubiriwa kwa hamu kubwa na kila mnyekundu na mweupe, kwani jezi mpya ni utambulisho wa utambulisho wa Simba kila msimu.
Awali, klabu kupitia taarifa zake rasmi, ilitangaza kuwa pazia la uzinduzi lingefunguliwa Alhamisi tarehe 28/8/25. Lakini kama ilivyo ada kwenye mambo makubwa, mabadiliko madogo yalibidi kufanyika. Inasemekana kuwa msambazaji rasmi wa jezi hizo, kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited, iliomba kusogeza mbele kidogo siku ili kuongeza mzigo mkubwa zaidi wa jezi. Hii ni habari njema kwa mashabiki, kwani maana yake ni kwamba hakuna atakayeachwa bila kupata jezi, iwe ni jijini, mikoani au hata visiwani.

Taarifa kutoka ndani ya klabu zinasisitiza kwamba shehena kubwa ya jezi tayari iko njiani kuwasili nchini. Wanunuzi wa jumla wamewekewa masharti – kila mmoja anatakiwa kuagiza si chini ya jezi 300 kwa mpigo, huku kila rangi ikienda kwa mamia yake. Hii ina maana moja tu: msimu huu Simba SC inakuja na rangi tatu tofauti za jezi, jambo linaloongeza msisimko wa mashabiki wanaopenda kuvaa uwanjani wakiwa na “identity” ya timu yao.
Lakini zaidi ya jezi, uzinduzi huu hautakuwa wa kawaida. Ni sherehe ya heshima, ya hadhi na burudani kwa kila shabiki atakayehudhuria. Kila tiketi ya kuingia itagharimu shilingi 250,000/=, gharama ambayo itajumuisha chakula cha kufa mtu na pia pea tatu za jezi mpya kabisa za msimu huu. Fikiria unarudi nyumbani na jezi tatu mpya mkononi, huku umeshiba na roho imetulia baada ya kushuhudia tukio kubwa la historia ya Simba.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Mashabiki tayari wameanza kupeana taarifa mitaani, mitandaoni na kwenye vijiwe vya soka. Kuna anayesema anasubiri kuona ubunifu mpya, kuna mwingine anatamani kuona kama jezi za msimu huu zitakuwa na mvuto ule ule wa Kiafrika unaoendana na hadhi ya Wekundu wa Msimbazi. Wengine wanasema tayari wameweka akiba kuhakikisha hawakosi tiketi, maana hii ni fursa ya kipekee – siyo tu kuvaa jezi, bali kuwa sehemu ya historia ya klabu yao pendwa.
Kwa Simba SC, kila msimu ni hadithi mpya, na jezi ndiyo jalada la hadithi hiyo. Mwaka huu, wadau wengi wanaamini klabu itazidi kuvunja rekodi, siyo tu uwanjani, bali pia katika namna ya kujitangaza na kujiweka kwenye ramani ya soka la kisasa barani Afrika. Tukio la Jumapili litakuwa kioo cha nguvu, umoja na mapenzi ya mashabiki kwa timu yao.
Kwa hiyo mashabiki wote, hakikisheni mnaweka tarehe hii kwenye kalenda zenu. Jumapili ya tarehe 31 Agosti, Masaki – The Super Dome, historia inaandikwa. Usibaki nyuma, vaa nyekundu na nyeupe, piga kelele zako, shangilia na usherehekee jezi mpya za Wekundu wa Msimbazi. Huu ndiyo wakati wa Simba, huu ndiyo msimu wa mapinduzi mapya!.