Klabu ya soka ya Fountain Gate Fc yenye makazi yake wilayani Babati mkoani Manyara imemtimua kocha wake raia wa Kenya Robert Matano kutokana na matokeo yasiyoridhisha katika ligi kuu ya Nbc nchini.
Matano alishindwana na mabosi wa klabu hiyo baada ya kumtimua hapo awali kutokana na kutoelewana kuhusu malipo ya fidia ambapo alirejea kikosini humo kuendelea na majukumu yake.
Hata hivyo sasa muafaka kamili imefikiwa baina ya pande hizo na sasa kocha huyo ameondoka kikosini humo na anasubiri kukamilisha baadhi ya taratibu za malipo kisha kuondoka nchini kurejea kwao nchini Kenya.
Kwa sasa kikosi hicho ambacho kimesaliwa na takribani michezo mitatu ya ligi kuu kipo chini ya makocha wasaidizi Amri Said na Khalid Adam.
Katika msimamo wa ligi kuu ya Nbc nchini klabu hiyo imecheza jumla ya michezo 27 ya ligi kuu ikiwa na alama 29 katika nafasi ya 12 ambapo wamesaliwa na michezo mitatu dhidi ya Jkt Tanzania na Coastal Union ambazo watakua ugenini huku dhidi ya Azam Fc watakua nyumbani katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati.