Site icon Sports Leo

Mayanga Kutua Mashujaa Fc

Klabu ya Mashujaa United imefanikiwa kumng’oa kocha Salum Mayanga katika klabu ya Mbeya City Fc kuja kuchukua nafasi ya ukocha mkuu klabuni hapo baada ya klabu hiyo kuachana na kocha Mohamed Barres kutokana na matokeo mabovu.

Mayanga alikuwa miongoni mwa makocha waliokuwa wakifukuziwa na uongozi wa Mashujaa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Bares na sasa ni rasmi atakuwa kocha mkuu wa kikosi hicho baada ya mabosi wa klabu hiyo kumalizana nae kimyakimya.

Chanzo cha kuaminika kutoka Mashujaa kimeithibitishia kuwa tayari wamemalizana na kocha huyo na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa rasmi ambapo kwa sasa anakamilisha taratibu za mwisho.

Mayanga kwa sasa anakinoa kikosi cha Mbeya City Fc na, hivi karibuni alikiongoza kuitoa Azam kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa mikwaju ya penalti 4-2, baada ya kutoka sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya Mashujaa zinaeleza kuwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu baina ya viongozi na kocha huyo, hatimaye yamekwenda vizuri na muda wowote jambo hilo litawekwa wazi.

“Mazungumzo yamekwenda vizuri Mayanga amepitishwa na viongozi kama chaguo linalofaa kuchukua nafasi ya Bares,” kimesema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.

Kwa upande wake, Mayanga amesisitiza kuwa hajafanya mazungumzo na timu yoyote na kwa sasa anabaki na Mbeya City ambayo malengo yake ni kuhakikisha anaipandisha Ligi Kuu Bara.

Exit mobile version