Klabu ya Simba Sc imefanikiwa kuchukua alama tatu muhimu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini dhidi ya Kmc baada ya kuifunga kwa mabao 2-1 katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini uliofanyika katika uwanja wa Kmc Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo kwa Simba sc sasa unamanisha kuwa klabu hiyo imeshinda mechi zake zote nne za viporo na kufanya tofauti ya alama baina yake na klabu ya Yanga sc katika msimamo wa ligi kuu ya Nbc nchini kuwa alama moja.
Simba sc ilianza kutanguliwa kufungwa mapema kwa bao la Rashid Chambo dakika ya 8 ya mchezo ambaye alipiga shuti kali la nje ya boxi la mita kumi na nane na kumshinda kipa Moussa Camara na kujaa wavuni.
Bao hilo lilidumu kwa dakika saba pekee ambapo dakika ya 15 mshambuliaji Steven Mukwala aliiachambua ngome ya Kmc na kufunga bao la kusawazisha ambapo pasi za haraka haraka za Kibu Dennis na Joshua Mutale zilimkuta mfungaji huyo na kufunga bao hilo.
Dakika ya ya 47 ya mchezo huo Mukwala alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi nzuri ya Joshua Mutale kwa mara nyingine na kuandika bao hilo la pili kwake na kwa Simba sc.
Mpaka dakika tisini za mwamuzi Henry Sasii zinakamilika Simba sc ilifanikiwa kuchukua alama zote tatu na kufikisha alama 69 katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kuu ya Nbc na sasa inaipumulia kwa karibu klabu ya Yanga sc yenye alama 70 kileleni mwa msimamo huo.