Simba Sc,Yanga Sc Katika Mission Nzito Afrika

Yanga Sc Yapangwa Kundi la Kifo,Simba Sc Kukutana na Vigogo Misri,Angola

by Dennis Msotwa
0 comments

Kahawa ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika mwaka 2025 imeanza kunukia! Droo iliyofanyika makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) nchini Misri imeacha gumzo kubwa  hasa kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania  baada ya timu mbili kongwe, Simba SC na Yanga SC, kupangwa katika makundi magumu yenye historia ndefu ya mafanikio barani.

Jumla ya timu 16 vigogo wa Afrika zimeingia hatua ya makundi, na kila moja ikitazamia kupenya hadi robo fainali. Kwa Tanzania, ni fahari kuona nembo mbili nyekundu na kijani zikipepea tena kwenye ramani ya soka la bara hili.

Simba Sc,Yanga Sc Katika Mission Nzito Afrika-Sportsleo.co.tz

SIMBA SC – KAZI KUBWA LAKINI INAWEZEKANA

banner

Wawakilishi wa Tanzania kutoka bonde la  Msimbazi, Simba SC, wamepangwa kwenye Kundi D pamoja na miamba ya soka la Afrika Petro Atlético ya Angola, Espérance de Tunis ya Tunisia na Stade Malien ya Mali.

Kwa macho ya mashabiki, kundi hili linaonekana kuwa na changamoto lakini pia fursa. Espérance ni timu yenye historia ya mataji, imekuwa ikitisha barani kwa miaka mingi. Wamepita mara nyingi katika hatua ya nusu fainali na fainali, wakitumia uzoefu wa kimataifa na nidhamu ya kiufundi wakiwa wametoka kucheza michuano ya kombe la dunia kwa ngazi ya klabu mwaka huu.

Petro Atlético, nao ni wenye uzoefu mkubwa katika mashindano haya. Uwanja wao wa Luanda ni moto wa kuotea mbali, na ndio watakuwa wenyeji wa Simba katika mchezo wa kwanza tarehe 21 Novemba mwaka huu.Kisha, kuna Stade Malien  timu ngumu, yenye wachezaji wa nguvu na nidhamu ya kiufundi.

Simba Sc,Yanga Sc Katika Mission Nzito Afrika-www.Sportsleo.co.tz

Lakini Simba imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka. Wamezoea presha ya michuano mikubwa na wameonyesha kwamba wanaweza kusimama imara mbele ya majina makubwa. Uwepo wa mastaa wenye uzoefu wa kimataifa, pamoja na kocha Dimitri Pandev mwenye mbinu za kisasa, unatoa matumaini mapya kwa mashabiki wa Msimbazi.

Mafanikio ya Simba yatategemea sana uwezo wa kupata pointi nyumbani kwa maana ya kuhakikisha kila timu itakayokuja Benjamin Mkapa Stadium inatoka mikono mitupu na kisha “kuiba” pointi chache ugenini ambapo wakifanikiwa hilo, Simba wana nafasi nzuri ya kutinga robo fainali kwa mara nyingine.

YANGA SC – KUNDI LA KIFO LAHITAJI UJASIRI

Kwa upande wa Yanga SC, mambo si mepesi. Wanabeba jina kubwa la Tanzania kwenye Kundi B ambalo limepachikwa jina la Kundi la Kifo ambapo hapa wanakutana na AS FAR Rabat ya Morocco, JS Kabylie ya Algeria, na bingwa wa kihistoria wa Afrika, Al Ahly SC ya Misri.

Kwa wapenzi wa soka, haya ni majina yanayotesha misuli,Al Ahly ni klabu yenye mataji mengi zaidi ya CAF Champions League  wanajivunia historia, uzoefu, na heshima ya kutisha. Kucheza dhidi yao ni mtihani wa kweli wa ubora.

Simba Sc,Yanga Sc Katika Mission Nzito Afrika-www.Sportsleo.co.tz

AS FAR Rabat, ambao watakuwa wageni wa kwanza wa Yanga kwenye mchezo wa ufunguzi, ni mabingwa wa zamani wa Afrika wenye nidhamu ya kiufundi na kasi ya wachezaji wa Morocco wakiwa wamemaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Rs Berkane katika ligi kuu ya Morocco msimu uliopita.
JS Kabylie, nao ni wazee wa michuano, wakijulikana kwa soka lenye akili na mbinu za Kiarabu za kaskazini ambazo huwakera wapinzani wengi.

Kwa Yanga, hii ni nafasi ya kuonyesha kwamba mafanikio ya miaka ya hivi karibuni hayakuwa bahati nasibu. Wanatakiwa kuingia kila mechi wakiwa na moyo wa ushindi, nidhamu, na kuamini uwezo wao.

Kama watashinda mechi za nyumbani na kupata angalau alama moja au mbili ugenini, wanaweza kupenya hadi hatua ya robo fainali kitu ambacho kingeingia kwenye historia ya klabu hiyo kwa mara ya kwanza katika michuano ya CAF Champions League.

UCHAMBUZI WA JUMLA – TANZANIA INAWEZA KUFANYA KITU

Michuano ya mwaka huu inatoa taswira mpya ya jinsi soka la Tanzania limepiga hatua kwani kwa mara ya pili mfululizo, klabu zetu mbili zimefika hatua ya makundi, jambo lililokuwa ndoto miaka michache iliyopita,Simba na Yanga sasa si washiriki tu ni wapinzani wanaochukuliwa kwa uzito na timu kubwa za Afrika.

Kinachotakiwa sasa ni maandalizi ya kiakili na kimwili. Ratiba ya CAF ni ngumu, safari ni ndefu, na uwanja wa ugenini ni tofauti. Lakini, kama kutakuwa na umoja kati ya timu, viongozi, na mashabiki hakuna kisichowezekana.

Simba inahitaji kutumia uzoefu wake wa kimataifa, na Yanga itahitaji moyo wa ushindi na nidhamu,Kwa vyovyote vile, hizi ni timu zenye hadhi mpya barani.

HITIMISHO – MUDA WA KUANDIKA HISTORIA MPYA

Kipenga cha kwanza kitakapolia tarehe 21 Novemba, macho yote yatakuwa kwa Dar es Salaam na Luanda,Yanga wakianza nyumbani dhidi ya AS FAR, watataka ushindi wa mwanzo kuamsha matumaini huku Simba, wakisafiri Angola, watataka matokeo chanya kuonyesha hawachezi kwa bahati.

Hii si tu michuano ya soka ni safari ya kuthibitisha kwamba Tanzania inaweza kusimama bega kwa bega na wakubwa wa Afrika na
Mashabiki wanatakiwa kujaza viwanja, kuimba kwa nguvu, na kuamini.Safari hii  iwe kwa Simba au Yanga historia mpya ya soka la Tanzania inaweza kuandikwa.

You may also like

Leave a Comment

Enable Notifications OK No thanks