Sports Leo

Simba Sc Yawaonya Mashabiki Vivuruge Caf

Kuelekea mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs, Klabu ya Simba SC yawaonya mashabiki wake kuepuka vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu vitakavyoweza kuigharimu klabu kwa adhabu kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumapili, Oktoba 26, 2025, kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, ambapo Simba itakuwa na jukumu la kukamilisha kazi baada ya kupata ushindi wa mabao 3–0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, alisema mashabiki wote wanakaribishwa kwa wingi kuishangilia timu yao, lakini wakumbuke kufuata sheria za mchezo na taratibu za CAF.

Simba Sc Yawaonya Mashabiki Vivuruge Caf-sportsleo.co,tz

“Tunawashukuru mashabiki wetu kwa kujitoa kwa hali na mali kulipia faini zilizotokana na adhabu zilizopita. Hata kama matoleo hayakuwa makubwa, klabu tutaongeza pale tulipobaki. Hata hivyo, ni marufuku kwa shabiki yeyote kuwasha moto au kuingia uwanjani. Haya ndiyo mambo mawili yaliyotuingiza kwenye adhabu mara ya mwisho,” alisema Ahmed.

Akaongeza kwa maneno mazito yaliyosindikizwa na tahadhari kali “Wapo watu wanaovaa jezi ya Simba lakini si mashabiki halisi. Wanakuja uwanjani kwa lengo la kuharibu. Tunawaonya kwamba mtu yeyote atakayefanya vitendo hivyo kwa makusudi tutamshughulikia papo hapo uwanjani. Simba haiwezi kufungiwa kwa upuuzi wa mtu mmoja.”

Ahmed alifafanua kuwa klabu imeshirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha mchezo huo unafanyika katika mazingira salama, huku akisisitiza kwamba mashabiki wajitokeze kwa wingi, lakini waonyeshe ustaarabu kama ilivyo desturi ya Wanasimba halisi.

Kuhusu viingilio, msemaji huyo alieleza kuwa “Kuelekea mchezo huu, tumeweka viingilio vya kitajiri. Tanzanite itakuwa Shilingi 250,000, Platinum 150,000, VIP A 30,000, VIP B 20,000, VIP C 10,000, na Mzunguko 5,000. Hii ni mechi kubwa inayoongeza hadhi ya klabu yetu, kwa hiyo kila Mwanasimba ana wajibu wa kulipa kiingilio chake.”Alisema kwa msisitizo mbele ya waandishi wa habari.

Akizungumzia umuhimu wa mchezo huo, Ahmed alisema mechi hiyo ni zaidi ya dakika 90 kwani inaleta heshima na thamani kwa Simba kama moja ya timu kubwa barani Afrika.

“Afrika hii, timu zilizocheza hatua ya makundi mara saba mfululizo ni Al Ahly na Mamelodi Sundowns, na sasa tunajiweka kwenye orodha hiyo. Tusije tukadharau mchezo huu. Hata kama tulishinda mabao matatu, tuutazame huu mchezo kama mpya. Haina maana tufungwe bao moja au mbili nyumbani, hilo halitakubalika.”

Msemaji huyo aliongeza kwa kuonyesha kujiamini kuhusu ubora wa kikosi cha sasa cha Simba “Tulikuwa tunapiga kelele kwamba Simba yetu haieleweki inavyocheza, lakini sasa imerejea. Simba ya kushambulia muda wote imerejea! Haya sio maneno ya kutoka usingizini, ni maneno ya kuona uhalisia. Mwalimu alisema uwanja wa kwanza ulikuwa mdogo, sasa Mkapa ni mkubwa. Njoo uone Simba ikifanya balaa zito.”

Ahmed pia hakusita kutamba akisema Simba ni timu pekee ya Tanzania iliyopata ushindi ugenini msimu huu wa CAF Champions League baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 ugenini siku ya jumapili.

“Zanzibar sio nje ya Tanzania, lakini kumbuka si rahisi kwenda Eswatini ukamtandika bingwa wa nchi yao mabao 3-0. Hilo ni jambo la kujivunia. Sasa kila Mwanasimba ana wajibu wa kuonyesha nguvu yake kwa kulipa kiingilio na kuishangilia timu.”Alisema Ahmed

Kocha mpya wa timu hiyo, Dimitar Pantev, anatarajiwa kuonekana kwa mara ya kwanza akisimama kwenye uwanja mkubwa wa Benjamin Mkapa, jambo linaloongeza hamasa kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo ambao watamuona kwa mara ya kwanza akisimama katika benchi la klabu hiyo maarufu nchini.

“Mwalimu amesema bado hajaridhika na kiwango cha timu, anataka zaidi. Nasi tunakwenda na kauli mbiu ya HATUJARIDHIKA, TUNATAKA ZAIDI!”alisema kwa majigambo msemaji huyo aliyejiunga na klabu hiyo akitokea kituo cha televisheni Azam Tv

Kwa maneno hayo, ni wazi kwamba Simba SC inajiandaa sio tu kwa ushindi, bali pia kwa kuonyesha taswira ya heshima, nidhamu na ubora wa kweli wa Wekundu wa Msimbazi — ndani na nje ya uwanja.

Exit mobile version