Kocha wa Simba sc Pablo Franco amesema kuwa Simba sc ni klabu bora kuliko Yanga sc kuelekea katika mchezo wa ligi kuu nchini baina ya timu hizo unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi April 30 saa 11 jioni katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba sc ikiwa ni mwenyeji wa mchezo huo inatarajiwa kukutana na Yanga sc yenye mabadiliko makubwa kiuchezaji tangu kocha Nasreddine Nabi ajiunge na timu hiyo huku ikifikisha mwaka mzima haijapoteza mchezo ambapo mara ya mwisho ilifungwa na Azam Fc April 26 mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu kuelekea mchezo huo Pablo amesema kuwa Simba sc ni bora na ina wachezaji wazuri kuliko watani zao Yanga sc japo wanaongoza ligi.
‘Tulikuwa na michuano ya kimataifa na wenzetu walikuwa na ligi pekee, unapoenda kwenye mechi kama hizi, unatamani kuwa na muda mzuri wa kujiandaa kama ilivyo kwa wapinzani wako lakini bado naamini tutafanya vizuri … ”
‘Ukiufuatilia mchezo wa kwanza tulikuwa bora kuliko wapinzani wetu, isingekuwa wao kugeuza mchezo kama mapigano na wangecheza mpira kama sisi pengine tungepata ushindi ,Wenzetu wana timu yenye ushindani lakini sisi tuna wachezaji bora zaidi kuliko wao na tunacheza mpira mzuri zaidi … ”
Pia kocha huyo alisifia kitendo cha mashabiki wa klabu hiyo kuja kuwapokea waliporejea nchini wakitokea Afrika ya Kusini walipopoteza mchezo wa robo fainali hatua ya klabu bingwa dhidi ya Orlando Pirates kwa matuta 4-3.
”Mashabiki wetu wana imani kubwa na sisi, sijawahi kuona popote timu inapoteza lakini tunarudi na kupokewa vizuri na mashabiki …. Hatuna presha na naamini utakuwa mchezo mzuri kwetu ”