Shirikisho la Soka nchini (TFF) limeamua kutumia waamuzi kutoka nje ya nchi katika mchezo wa ligi kuu ya soka ya Nbc nchini baina ya Yanga sc dhidi ya Simba sc utakaofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya jumatano Juni 25 2025.
Mchezo huo maarufu kama Dabi ya Kariakoo kati ya timu hizo utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Misri na Somalia pamoja na mmoja kutoka Tanzania.
Mwamuzi wa kati atakuwa ni Amin Mohammed Omari huku msaidizi namba moja atakuwa Mahmoud Ahmed na msaidizi namba mbili ni Samir Saad Mohamed na Ofisa namba nne anatarajiwa kuwa Alli Mohammed kutoka nchini Somalia.
Pamoja na waamuzi hao kutoka nje pia Shirikisho la soka nchini limemtangaza Salim Omary Singano kutoka Tanga kuwa Kamishna wa mchezo huo.
Sababu kubwa ya kutumia waamuzi hao inatajwa kuwa ni presha ya mchezo huo kwa waamuzi wa ndani ambao wengi wamekua waoga kufanya maamuzi hasa kwenye matukio muhimu katika mchezo huku pia ikitajwa lengo jingine ni kutoa fursa kwa waamuzi wa ndani kujifunza zaidi.
Mchezo huo ndio utaamua bingwa wa ligi kuu nchini ambapo sasa katika msimamo wa ligi Yanga sc anaongoza akiwa na alama 78 dhidi ya 77 za Simba sc na endapo atapoteza mchezo huo basi Simba Sc itakua bingwa wa ligi kuu msimu wa 2024-2025.