Mabao 4-01 yametosha kuiongezea uimara Klabu ya Yanga SC kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuibuka na ushindi mnono dhidi ya KMC FC katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo pia umeendelea kuipa motisha timu hiyo chini ya Kocha wake mpya, Pedro Miguel Gonçalves, ambaye ameonekana kuanza safari yake vizuri ndani ya Wananchi tangu kuchukua mikoba ya Roman Folz aliyetimuliwa kutokana na mwenendo mbovu wa kikosi hicho katika michuano ya kimataifa.
Katika mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki wengi wa soka, Yanga SC ilianza kwa kasi na kuonyesha umahiri mkubwa wa kushambulia huku safu yao ya kiungo ikimiliki mchezo kwa asilimia kubwa. Kipa wa KMC alilazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia juhudi za washambuliaji wa Yanga ambao waliokuwa wakiongozwa na Pacome Zouzoua, Prince Dube na Maxi Nzegeli.
Bao la kwanza lilipatikana dakika ya 36, baada ya mshambuliaji hatari wa Yanga, Maxi Nzegeli, kukamilisha vyema pasi safi iliyopangwa kwa ustadi na Pacome Zouzoua. Bao hilo liliamsha shangwe kubwa katika benchi la Yanga na miongoni mwa mashabiki waliokuwa wamejitokeza kuishangilia timu yao.
Hata hivyo, furaha hiyo ya Yanga haikudumu kwa muda mrefu sana, kwani dakika ya 42 KMC walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wao Daruweshi Saliboko aliyemalizia mpira uliotoka katika mikono ya kipa Djigui Diarra langoni mwa Yanga SC. Bao hilo lilionekana kuiamsha zaidi Yanga ambayo ilionekana kutoridhishwa na kwenda mapumziko ikiwa sare.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa hasa kwa upande wa Yanga SC ambao walionekana kurejea uwanjani wakiwa na malengo ya kuwapa mashabiki wao ushindi muhimu.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Hatimaye dakika ya 72, Zouzoua aliandika bao la pili kwa Wananchi baada ya kumalizia kwa ustadi pasi ya beki mshambuliaji Israel Mwenda, akiutupa mpira nyavuni kwa shuti kali lililoenda moja kwa moja upande wa juu wa goli la KMC.
Mageuzi ya kocha Gonçalves yalianza kuonekana zaidi alipomtoa Prince Dube na kumwingiza Andy Boyeli, mabadiliko yaliyokuja kuzaa matunda ndani ya muda mfupi. Boyeli alilitia mwanga lango la KMC dakika ya 82 kupitia mkwaju wa penalti uliotolewa baada ya beki wa KMC kumvuta mshambuliaji huyo ambaye Kwa utulivu mkubwa, alimtungua kipa na kuipeleka Yanga mbele kwa tofauti ya mabao 3-1.
Dakika ya 90+3 zilikuwa kama muhuri wa ushindi, Boyeli tena akifunga bao la nne baada ya kuunganisha pasi maridadi ya Celestine Echúa. Bao hilo lilizidi kuzamisha matumaini ya KMC kurejea mchezoni, huku Wananchi wakizidi kushangilia ubabe wao jijini Dar es Salaam.
Hadi dakika 90 zinakamilika, Yanga SC iliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0, ushindi ambao umeendeleza rekodi yao nzuri katika mchezo wa pili mfululizo chini ya Gonçalves. Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 10 katika michezo minne, ikikalia kinara wa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC. Kwa upande mwingine, KMC imedumu mkiani ikiwa na pointi 3 pekee baada ya kucheza michezo sita, hali inayoongeza shinikizo kwa Kocha Marcio Maximo ambaye bado hajapata mwelekeo sahihi katika kikosi chake.
Mashabiki na wachambuzi wa soka nchini wanaamini kuwa kiwango kilichooneshwa na Yanga ni ishara ya kuimarika kwa timu hiyo ambayo msimu huu imejipanga kurejesha heshima yake katika michuano ya ndani na kimataifa. Kocha Gonçalves amesikika mara kadhaa akisisitiza nidhamu ya mchezo na kuendelea kuongeza ushindani wa namba katika kikosi chake, jambo linalotarajiwa kuibeba Yanga zaidi msimu huu.
Kwa matokeo haya, Wananchi wanaonekana kujihakikishia mwanzo mzuri wa ligi, huku presha ikiendelea kuongezeka kwa timu zinazowafuatia katika mbio za ubingwa wa msimu wa 2025/26.



