Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kufuzu hatua ya Fainali ya michuano ya kombe la Muungano nchini baada ya kuifunga Zimamoto Fc kwa mabao 3-1 kwa penati baada ya kutoka sare ya 1-1 katika dakika tisini za kawaida.
Mchezo huo umefanyika katika uwanja wa Gombani Visiwani Pemba na kushuhudiwa na mashabiki wengi licha ya mvua kubwa iliyonyesha uwanjani hapo.
Yanga sc sasa itavaana na Jku ambayo iliifunga Azam Fc kwa mabao 2-1 siku ya jana katika fainali hizo zitakazochezwa wikiendi ijayo.
Yanga sc ilianza kupata bao kupitia kwa Maxi Nzengeli dakika ya 28 kwa shuti kali akimalizia pasi safi ya Mudathir Yahaya lakini bao hilo lilisawazishwa dakika ya 70 kwa penati na Said Mwinyi baada ya AbouTwalib Mshery kufanya makosa na kusababisha faulo ndani ya eneo la hatari.
Pamoja na Yanga sc kushambulia mara nyingi lakini walishindwa kupata bao na kuufanya mchezo kwenda matuta baada ya dakika tisini za mwamuzi.
Katika matuta hayo kipa AbouTwalib Mshery aliibuka shujaa baada ya kuokoa michomo miwili ya Zimamoto Fc huku mmoja ukigonga mwamba na kuifanya Yanga sc kupata ushindi wa 3-1 na kufuzu fainali za michuano hiyo ambapo itacheza na Jku wikiendi hii.