Ijumaa hii, Oktoba 10, Viwanja vya Posta, Kijitonyama vitageuka kuwa uwanja wa vita wakati ngumi zitakapopigwa kwa kishindo, huku mashabiki wakitarajiwa kushuhudia mapambano ya kusisimua yatakayowakutanisha mabondia wakali wa ndani na nje ya nchi. Jumla ya mapambano nane yamepangwa kufanyika, yakihusisha mikanda miwili ya kimataifa ambayo itagombaniwa usiku huo wa kihistoria.
Pambano kuu linalosubiriwa kwa hamu kubwa litawakutanisha bondia machachari wa Tanzania, Juma Choki, dhidi ya Manikandan V kutoka India, katika pambano la uzani wa super bantam. Hili ndilo litakuwa pambano la kulipiza kisasi kwa Choki, ambaye kwa sasa amerudi na moto mpya baada ya kushiriki mashindano makubwa ya Dunia hivi karibuni.
Juma Choki, ambaye ni miongoni mwa mabondia wanaopanda chati kwa kasi Afrika Mashariki, amesema amejiandaa vilivyo kwa pambano hilo na yuko tayari kupigania ushindi mbele ya mashabiki wake wa nyumbani. “Nimerudi nikiwa na uzoefu mkubwa na najua mashabiki wanataka ushindi. Nitapambana hadi mwisho kuhakikisha mikanda inabaki Tanzania,” alisema Choki kwa kujiamini.
Kwa upande wake, Manikandan V kutoka India si bondia wa kubezwa. Ni bondia mwenye uzoefu mkubwa kimataifa, mwenye rekodi nzuri na uwezo wa kupigana raundi zote kwa kasi na umakini. Ujio wake nchini umeongeza mvuto wa pambano hilo, hasa ikizingatiwa kuwa atakuwa akiwania mkanda wa kimataifa wa WBC Silver Africa.
Waandaaji wa pambano hilo wamesema maandalizi yote yamekamilika na viingilio vimepangwa kuwa rafiki ili kila mpenzi wa ndondi aweze kuhudhuria. “Tumelenga kutoa burudani ya hali ya juu. Tunawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia mashindano ya kiwango cha juu kabisa,” alisema mmoja wa waandaaji.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Mbali na pambano la Choki, kutakuwa na mapambano mengine saba ya utangulizi yatakayohusisha mabondia wa ndani kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Wengine watakaopanda ulingoni ni pamoja na ibrahim mafia dhidi ya Abdulrahman Magoma katika moja ya mapambano ya utangulizi.
Ni wazi kuwa jiji la Dar es Salaam litakuwa sehemu ya historia nyingine ya ndondi Ijumaa hii, huku mashabiki wakitarajia vitasa kulia, na glovu kuamua nani ni mfalme wa ulingo. Mashabiki wameaswa kuwasili mapema kupata nafasi nzuri za kushuhudia mapambano hayo makali.