Sports Leo

AZAM FC YATINGA HATUA INAYOFUATIA KWA USHINDI WA KISHUJAA DHIDI YA EL MERRIEKH BENTIU

Klabu ya Azam FC imeendeleza makali yake katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya El Merrekh Bentiu ya Sudan, katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam. Ushindi huo unaifanya Azam kufuzu kwa kishindo hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 4-0, kufuatia ushindi wa awali wa mabao 2-0 walioupata ugenini nchini Sudan.

Katika mchezo wa leo, Azam FC ilionyesha udhibiti mkubwa wa mchezo tangu dakika za mwanzo, wakitumia faida ya uwanja wa nyumbani na morali ya ushindi walioupata katika mchezo wa kwanza. Mashabiki wachache waliopata nafasi ya kuingia walionekana kushangilia kila dakika timu yao ilipokuwa ikisogea langoni mwa wapinzani. Dakika ya 18, Yoro Diaby alifungua ukurasa wa mabao kwa kichwa safi akiunganisha kona murua ambapo Bao hilo liliwapa Azam ujasiri mkubwa na kuwafanya kuendelea kushambulia kwa spidi na nidhamu kubwa.

AZAM FC YATINGA HATUA INAYOFUATIA KWA USHINDI WA KISHUJAA DHIDI YA EL MERRIEKH BENTIU-Sportsleo.co.tz

Licha ya El Merrekh Bentiu kujaribu kusawazisha kwa kutumia mashambulizi ya kushtukiza, walikumbana na ukuta imara wa mabeki wa Azam FC, wakiongozwa na Yeison Fuentes na Yoro Diaby ambao walihakikisha hakuna upenyo kwa wageni hao. Kipa Issa Fofana naye alisimama imara kila alipojaribiwa, na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi, huku kocha Florent Ibenge akionekana kuhamasisha wachezaji wake kuongeza umakini na kushambulia kwa ufanisi. Azam FC walipoteza nafasi kadhaa za wazi kupitia kwa Feisal Salum na Nassoro Saiduni lakini jitihada zao hazikuisha. El Merrekh walionekana kudhoofika kadri dakika zilivyoongezeka kutokana na uchovu na presha ya mchezo.

Hatimaye, katika dakika za majeruhi (90+2), Nassoro Saiduni alihakikisha Azam wanaondoka na ushindi mnono baada ya kufunga bao la pili kwa kichwa kali ndani ya boksi, akimalizia mpira wa kurudi uliotokana na shambulizi lililoongozwa kutokea upande wa kulia. Bao hilo liliamsha shangwe kubwa ndani ya Chamazi na kuwaweka Azam FC katika nafasi salama ya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-0.

Kwa matokeo haya, Azam FC sasa wanakwenda kukutana na KMKM ya Zanzibar katika hatua inayofuata ya michuano hii. Hii inatarajiwa kuwa ni mchezo wa kuvutia kwani timu hizo mbili za ukanda wa Afrika Mashariki zitakutana kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano ya kimataifa. Wapenzi wa soka wanatarajia pambano la majirani litakalopamba moto na kuongeza ladha ya ushindani.

Kocha Florent Ibenge amepongeza wachezaji wake kwa nidhamu, mshikamano na ubora waliouonyesha, akisema kuwa mafanikio haya ni matunda ya maandalizi mazuri na mshikamanifu wa kikosi kizima. Mashabiki nao wameanza kuota ndoto kubwa ya kuona Azam wakifika mbali zaidi, hasa kwa kuzingatia aina ya kikosi imara kilichojaa vijana wenye vipaji na uzoefu wa kutosha.

Kwa jumla, Azam FC wameonesha kuwa ni timu yenye ndoto kubwa barani Afrika. Safari yao sasa inaelekea Zanzibar, lakini lengo kubwa ni kuhakikisha wanapiga hatua hadi makundi na kuendelea kuipa heshima Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Exit mobile version