Klabu ya Simba sc imefanikiwa kuchukua alama tatu muhimu mbele ya Azam Fc baada ya kuifunga 3-0 katika mchezo wa ligi kuu ya soka ya Nbc uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba sc iliyoingia katika mchezo huo bila matumaini ya ushindi ilijitahidi kuzuia isifungwe hasa kipind cha kwanza na Azam Fc iliyosheheni mastaa kama Kipre Jr,Feisal Salum na Gibril Sillah huku yenyewe ikiwakosa mastaa wake Saido Ntibanzokiza,Cletous Chama,Luis Miqquisone na Henock Inonga ambaye alianzia benchi.
Azam Fc pamoja na kufanya mashambulizi mara kwa mara lakini uimara wa kipa Ayoub Lakred uliwaweka Simba sc mchezoni huku Feisal Salum akikosa penati dakika ya 35 ya mchezo huo na kufanya mpaka mapumziko matokeo kusalia suluhu.
Kipindi cha pili Simba sc iliamka na kufanikiwa kupata mabao matatu yaliyofungwa na Sadio Kanoute dakika ya 63 na bao la kichwa la Fabrice Ngoma dakika ya 77 ya mchezo huku David Kameta akifunga bao la tatu dakika ya 89 ya mchezo.
Pamoja na ushindi huo Simba sc imeendelea kusalia katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu nchini ikiwa na alama 56 huku Azam Fc ikiwa nafasi ya pili kwa alama 57 na Yanga sc ikiwa kileleni kwa alama 68 katika michezo 26 ya ligi kuu nchini.