Site icon Sports Leo

Taifa Stars Yapigwa 2-0 na Iran

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeendelea kusuasua kwenye medani ya kimataifa baada ya kupoteza mchezo wake wa nne mfululizo, kufuatia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Iran katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa leo Jumanne, Oktoba 14, mjini Dubai, Falme za Kiarabu.

Katika mchezo huo uliolenga kuiweka Stars kwenye hali ya ushindani kuelekea mechi zijazo za kufuzu Kombe la Dunia na AFCON, kikosi hicho kilionekana kutojiamini na kushindwa kulinda nidhamu ya mchezo dhidi ya wapinzani wao waliowazidi kila idara. Mabao ya Iran yalifungwa kila kipindi, na kuacha Stars ikihaha kurekebisha hali bila mafanikio.

Huu ni mwendelezo wa matokeo mabaya kwa kikosi cha kocha Hemed Morocco, ambaye amekuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini kufuatia mwenendo wa timu kuwa wa kutoridhisha tangu aingie madarakani mapema mwaka 2024.

Tanzania ilianza kuyumba baada ya kutolewa kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN 2024, ambapo ilifungwa bao 1-0 na Morocco. Baada ya hapo, Stars ilicheza michezo miwili ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Niger na Zambia, na kupoteza yote kwa matokeo ya mabao 2-0 kwa kila mchezo. Kichapo hiki kutoka kwa Iran kimeifanya Tanzania kupoteza mechi nne mfululizo bila kufunga bao hata moja.

Kwa mashabiki na wachambuzi wa soka, hali hii inaibua maswali mengi kuhusu uwezo wa timu na mustakabali wa kocha Hemed Morocco katika benchi la ufundi. Licha ya kupewa matumaini makubwa wakati wa uteuzi wake, bado kocha huyo anaonekana kushindwa kuipa timu mwelekeo sahihi wala mwendelezo wa ushindani waliouonesha kipindi kifupi kilichopita.

Katika mchezo wa leo, Stars ilionekana kuwa na mapungufu makubwa katika eneo la kiungo, kukosa ubunifu na kushindwa kutengeneza nafasi za kufunga. Safu ya ulinzi pia haikuwa imara, huku Iran wakitumia uzoefu wao vizuri kutawala mchezo na kuhitimisha kwa ushindi wa uhakika.

Kwa sasa, presha inazidi kuongezeka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua hatua madhubuti kuhusu hatma ya benchi la ufundi na mipango ya maendeleo ya timu ya taifa. Wadau wengi wameshaanza kupaza sauti zao wakitaka mabadiliko ya haraka, wakidai kuwa muda unayoyoma na hakuna dalili za maboresho.

Pia kuna hofu kuwa kama hali haitabadilika haraka, Tanzania inaweza kujikuta ikipoteza nafasi nyingine ya kushiriki michuano mikubwa kama AFCON na Kombe la Dunia kwa mwaka 2030 kwani la mwakani 2026 tayari timu imeshindwa kufuzu, licha ya kuwa na kikosi chenye vipaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Mchezo huu dhidi ya Iran, ambao ulitarajiwa kuwa kipimo kizuri kwa Stars, sasa umegeuka kuwa kengele ya tahadhari kwa TFF na benchi la ufundi. Mashabiki wanataka mabadiliko si tu ya matokeo, bali pia ya mfumo mzima wa maandalizi ya timu ya taifa, ikiwemo uwekezaji kwenye wachezaji wa ndani, mbinu za kisasa na maandalizi ya muda mrefu.

Kwa sasa, macho yote yatakuwa kwa Stars kwenye mchezo wao ujao, huku swali kuu likibaki: je, Hemed Morocco ataweza kugeuza mwelekeo wa timu na kurejesha imani ya Watanzania? Au huu ndio mwanzo wa mwisho wa muda wake na timu ya taifa? Wakati ndio utakaotoa majibu.

Exit mobile version