Site icon Sports Leo

Yanga Kumtangaza Romuald Rakotondrabe Kuwa Kocha Mpya, Folz Kuvunjiwa Mkataba

Klabu ya Yanga SC imekamilisha usajili wa kocha mpya, Romuald Rakotondrabe, raia wa Madagascar, ambaye sasa atachukua rasmi nafasi ya Romain Folz, aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo tangu mwanzoni mwa msimu wa 2024/2025. Uongozi wa Yanga umekaribia kumtangaza Rakotondrabe na atasaini mkataba wa miaka miwili, huku mchakato wa kuvunja mkataba wa Folz ukiwa katika hatua za mwisho.

Kocha Rakotondrabe mwenye umri wa miaka 60, ni jina linalotambulika sana katika medani ya soka barani Afrika, hasa kutokana na mafanikio yake akiwa na timu ya Taifa ya Madagascar. Kivutio kikubwa katika wasifu wake ni mafanikio makubwa aliyoyapata katika michuano ya CHAN (African Nations Championship) ambayo ilifanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Akiwa na kikosi kisicho na wachezaji wa kulipwa kutoka nje ya nchi, aliweza kuiwezesha Madagascar kufika hatua ya fainali, jambo lililompa heshima kubwa kwenye soka la Afrika Mashariki na Kati.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu, Mabosi wa Yanga Sc imevutiwa na falsafa ya uchezaji ya Rakotondrabe ambayo inasisitiza nidhamu ya kiuchezaji, kushambulia kwa mpangilio, na matumizi ya vipaji vya ndani ya timu. Uongozi umeeleza kuwa uteuzi wake ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuendeleza falsafa ya soka inayotegemea uchezaji wa kuvutia lakini pia wenye matokeo chanya.

Wakati huo huo, mustakabali wa Romain Folz, raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 35, upo ukingoni. Ingawa alipokelewa kwa matumaini makubwa kutokana na uzoefu wake katika soka la Afrika akiwa amewahi kuzinoa timu kama AmaZulu na Marumo Gallants za Afrika kusini, mafanikio yake na Yanga yamekuwa ya kusuasua. Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya matokeo yasiyoridhisha na tofauti za kimkakati kati yake na baadhi ya viongozi wa juu wa klabu ni miongoni mwa sababu zilizochangia hatua ya kuvunjwa kwa mkataba wake.

Uongozi wa Yanga, kupitia kwa Afisa Habari wake, umetilia mkazo kuwa bado una imani na Folz lakini hiyo ni kama danganya toto ambapo za ndani zaidi ni kuwa klabu hiyo ipo katika mchakato huo wa chini chini kuachana na kocha huyo na kumtangaza Roro kama kocha mpya ambapo atakuja na benchi lake la ufundi.

“Tumefanya tathmini ya kina kuhusu mwenendo wa timu na tukaona tuna imani na kocha Folz,Tunaamini Folz ataongeza thamani kubwa kwa klabu yetu kwa kuendeleza vipaji tulivyonavyo na kuongeza ushindani,” alisema msemaji wa klabu hiyo.

Mashabiki wa Yanga wamepokea habari hizi kwa hisia tofauti. Wengine wameonesha matumaini mapya kwa ujio wa Rakotondrabe, wakiamini uzoefu wake kwenye soka la Afrika unaweza kuwa suluhisho la changamoto zilizokuwepo, huku wengine wakieleza imani yao kwa Folz, ambaye licha ya misukosuko, ameweza kuonesha mwanga katika baadhi ya mechi.

Yanga SC sasa inatarajiwa kuingia katika ukurasa mpya wa historia yake, ikiwa na matarajio ya kuona mabadiliko chanya ndani ya kikosi ambapo kwa kocha Rakotondrabe, huu ni mwanzo wa safari mpya katika soka la Tanzania, huku macho yote ya mashabiki wa soka yakielekezwa kwake kuona kama ataweza kuendeleza mafanikio ya klabu hiyo kongwe nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu, kocha huyo mpya anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania mwishoni mwa wiki hii, ambapo ataungana na kikosi hicho kuanza maandalizi ya mechi zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kampeni za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Exit mobile version