Yanga Sc Yahamia Zanzibar Caf

Yapakimbia B/mkapa Ikihaha Kufuzu Robo Fainali

by Dennis Msotwa
0 comments

Klabu ya Yanga Sc imeamua kuandika historia mpya katika soka la Tanzania baada ya kuthibitisha  kwamba mechi zake zote za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League 2025/26) zitachezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Uamuzi huo umetangazwa rasmi na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, ambaye amesema kwamba ni hatua ya kimkakati iliyopitishwa baada ya tathmini ya kina iliyofanywa na uongozi wa klabu kufuatia droo ya makundi ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Yanga Sc Yahamia Zanzibar Caf-www.sportsleo.co.tz

KUNDI LA KIFO LAKUTANISHA YANGA NA MASTAA WA AFRIKA

banner

Yanga imepangwa katika Kundi B, kundi linalojumuisha majina makubwa katika soka la Afrika ikiwemo Al Ahly SC ya Misri (mabingwa wa kihistoria wa CAF), AS FAR Rabat ya Morocco (mabingwa wa zamani wa bara), na JS Kabylie ya Algeria, moja ya vilabu vyenye historia ndefu katika soka la Kaskazini mwa Afrika.

Ni kundi lililobatizwa jina la “Kundi la Kifo” kutokana na ubora na ukubwa wa vilabu vilivyomo ndani yake,Kamwe anasema, hata ndani ya klabu ya Yanga, hakuna aliyejaribu kulificha hilo kundi ni gumu, lakini nalo ndilo linalowapa hamasa kubwa zaidi.

“Ukiangalia kundi hili ambalo lina timu nne, kila mmoja anayefuatilia soka la Afrika anajua ni kundi gumu. Hili ndilo kundi la kifo,” alisema Kamwe akiwa na tabasamu la kujiamini.

“Sio kundi jepesi, sio kundi lelemama. Lakini sisi kama Yanga tunakiri kwamba hii ni changamoto tuliyokuwa tukiisubiri. Hatutaki kuwa washiriki, tunataka kuwa washindani.”Alimalizia kusema

Kwa mujibu wa ratiba rasmi iliyotangazwa na CAF, Yanga itaanzia kampeni zake nyumbani dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco kabla ya kusafiri hadi Algeria kuivaa JS Kabylie katika mchezo wa pili wa kundi hilo.

Yanga Sc Yahamia Zanzibar Caf-www.sportsleo.co.tz

KWANINI ZANZIBAR? HII NDIO SABABU YA MSINGI

Swali lililowapata mashabiki wengi ni: kwa nini Yanga imeamua kuhamishia makao yake ya nyumbani Zanzibar, badala ya kuendelea kucheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam?

Kamwe amesema uamuzi huo haujafanywa kwa hisia, bali ni sehemu ya mkakati wa kuongeza nguvu ya kiufundi na kisaikolojia kwa wachezaji na mashabiki.

“Tumeangalia mazingira, hali ya hewa, ubora wa uwanja na hali ya mashabiki. Uwanja wa New Amaan Complex una ubora mkubwa sana wa kimataifa na unatoa mazingira bora kwa wachezaji wetu kucheza soka la kuvutia,” alisema Kamwe.

Yanga Sc Yahamia Zanzibar Caf-www.sportsleo.co.tz

Uwanja huo, uliokarabatiwa kwa viwango vya FIFA, unatarajiwa kuwa moja ya viwanja bora zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki. Yanga wanatarajia kutumia hali ya hewa ya visiwani Zanzibar na upepo wa Bahari Hindi kama silaha ya kisaikolojia dhidi ya wapinzani wao kutoka Afrika Kaskazini.

Aidha, Kamwe amewatupia chambo mashabiki wa Zanzibar, akiwataka wajitokeze kwa wingi kuipokea timu hiyo.

“Tunawaambia mashabiki wa Zanzibar, jiandaeni. Yanga inakuja nyumbani kwenu. Mechi tatu zote za makundi tutacheza New Amaan Complex. Hii ni nafasi ya kihistoria — Zanzibar sasa itakuwa sehemu ya safari ya Yanga kuelekea mafanikio ya Afrika,” aliongeza Kamwe.

TATHMINI YA UAMUZI HUU – STRATEGY YA KIBONGO YA KIMATAIFA

Kwa wachambuzi wa soka, hatua ya Yanga kucheza visiwani Zanzibar inaonekana kama mkakati wa kimkakati zaidi kuliko wa kihisia.
Kwa muda mrefu, timu nyingi za Afrika zimekuwa zikihamishia mechi zao nyumbani kwenye viwanja vyao visivyozoeleka na wapinzani ili kupata faida ya kisaikolojia.

Zanzibar ni mazingira tofauti kabisa na Dar es Salaam — hali ya hewa ya baharini, mashabiki wa moto na upepo unaoweza kubadilisha mchezo,Kwa wapinzani kama Al Ahly au AS FAR, ambao wamezoea viwanja vya baridi vya Cairo na Rabat, kucheza katika joto la visiwani inaweza kuwa changamoto kubwa.

Pia, uwanja wa New Amaan Complex una mandhari mpya ya kisasa na nyasi laini zenye ubora wa kimataifa  kitu ambacho kinaweza kuwapa Yanga fursa ya kucheza soka la pasi fupi na la kuvutia, mtindo wanaoupenda.

MALENGO YA YANGA – KUFIKA ROBO FAINALI

Kamwe amesisitiza kuwa malengo ya Yanga msimu huu si kushiriki tu, bali kufika hatua ya robo fainali na kuvunja rekodi ya historia yao katika michuano ya CAF Champions League.

“Tunataka kuwa moja ya timu mbili kutoka kundi hili zitakazofuzu robo fainali. Tunajua si rahisi, lakini tumeanza maandalizi mapema,” alisema.

Taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi zinaeleza kuwa Yanga imeanza mipango ya kambi maalum ya mazoezi visiwani humo ili kuzoea mazingira mapema kabla ya mchezo wa kwanza dhidi ya AS FAR Rabat.

ZANZIBAR KUWAKA MOTO

Kwa sasa, macho yote ya mashabiki wa soka nchini yameelekezwa Zanzibar,New Amaan Complex inatarajiwa kugeuka kiwanja cha historia, huku mashabiki wa Yanga kutoka Tanzania Bara na Visiwani wakitarajiwa kumiminika kwa wingi.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano ya CAF, visiwa vya Zanzibar vitakuwa mwenyeji wa mechi za hatua ya makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hii ni hadithi mpya ya Yanga hadithi ya ujasiri, ubunifu na mipango ya kitaalamu.
Kama watafanikiwa kuutumia vyema uwanja huo na nguvu za mashabiki wa Zanzibar, Yanga inaweza kuandika ukurasa mpya wa fahari ya Tanzania katika ramani ya soka la Afrika.

You may also like

Leave a Comment

Enable Notifications OK No thanks