Klabu ya Azam FC imeanza msimu mpya wa Ligi Kuu NBC Tanzania Bara kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City FC katika mchezo wa kwanza uliopigwa leo kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Chini ya Kocha Mkuu Florent Ibenge, Wanalambalamba walionyesha kiwango cha kuvutia na kutuma ujumbe kwa wapinzani wao kuwa msimu huu wana malengo makubwa ya kutwaa taji la ligi.
Azam FC walianza mchezo kwa kasi wakimiliki mpira na kushambulia kwa nidhamu huku kiungo wao wa kati ukiongozwa na Feisal Salum “Fei Toto”, aliyekuwa kiungo hai akipanga mashambulizi. Wapinzani wao, Mbeya Fc walijaribu kuhimili shinikizo kwa kuzuia mashambulizi ya haraka, lakini hawakuweza kuzuia nguvu ya kikosi kipya cha Ibenge kilichokuwa na morali kubwa.
Bao la kwanza lilipatikana dakika ya 32 baada ya shambulizi lililoanzia upande wa kulia na mshangao wa AAzam Abdul Sopu alitoa krosi murua ndani ya eneo la hatari na Nassoro Saiduni akapanda juu ya mabeki wa Mbeya City na kupiga kichwa safi kilichomshinda kipa Benno Kakolanya na kujaa wavuni. Bao hilo liliwasha moto wa mashabiki wa Azam waliokuwa wakishangilia kwa nguvu wakifurahia mwanzo mzuri wa msimu.
Baada ya bao hilo, Mbeya City Fc walijaribu kujibu kwa kushambulia kwa kushitukiza, lakini walikosa umakini mbele ya lango la Azam FC. Kipa wa Azam Fc Issa Fofana alifanya kazi nzuri kuhakikisha timu inakwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi na ndani ya dakika ya 46, Azam waliongeza bao la pili. Shambulizi kali lililoongozwa na Feisal Salum lilimfanya kipa Benno Kakolanya kuokoa mpira uliokuwa unaelekea wavuni, lakini mpira ukamponyoka na kuangukia miguu ya Feisal ambaye hakukosea, akautumbukiza wavuni kwa ustadi na kuwapa Wanalambalamba uongozi wa mabao 2-0.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Baada ya bao hilo la pili, Azam waliendelea kutawala mchezo kwa utulivu, wakicheza kwa kujiamini huku wakilinda uongozi wao. Mbeya City walijaribu kurejea mchezoni kwa mashambulizi ya haraka, lakini walishindwa kuipenya safu ya ulinzi ya Azam iliyokuwa imara chini ya uongozi wa mabeki wake wa kati Yeison Fuentes na Yoro Diaby waliocheza kwa nidhamu kubwa.
Mashabiki wa Azam walionekana kufurahia falsafa mpya ya Kocha Florent Ibenge, ambaye aliwaongoza wachezaji wake kucheza soka safi la pasi na mashambulizi ya kasi. Ushindi huu wa 2-0 umewapa Azam FC pointi tatu muhimu na mabao mawili ya kufunga bila kuruhusu goli, jambo linalowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa awali wa ligi.
Kwa matokeo haya, Azam FC wameanza msimu kwa morali kubwa na kuonyesha dhamira ya kupambana na vigogo wa ligi kama Yanga SC na Simba SC. Mashabiki wa klabu hiyo wanatarajia kuona timu ikiendeleza kiwango hiki bora katika michezo inayofuata ili kudhihirisha uwezo wa benchi jipya la ufundi chini ya Ibenge na wachezaji wapya waliojiunga kuongeza nguvu.