Home Makala 250K Kushuhudia Uzinduzi wa Jezi Simba Sc

250K Kushuhudia Uzinduzi wa Jezi Simba Sc

by Dennis Msotwa
0 comments

Klabu ya Simba sc imetangaza kuwa uzinduzi wa jezi za klabu hiyo kwa ajili ya msimu huu utafanyika Agosti 27 mwaka huu katika ukumbi wa Superdome uliopo masaki jijini Dar es salaam ambapo tukio hilo litahudhuriwa na wasanii mbalimbali huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa mmoja kati ya wakongwe wa soka barani Afrika.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Meneja wa Mawasiliano na habari wa klabu hiyo alisema kuwa uzinduzi wa mwaka huu utakua wa aina yake na mashabiki watakaopenda kuhudhuria watalipia kiasi cha shilingi 250,000/= ambayo pia watapata jezo zote tatu za msimu huo pamoja na burudani zingine ukumbini.

“Kwa ambao wanahitaji kuhudhuria kwenye tukio letu la Super Dome ambalo lina idadi maalumu, apige kwenye namba 0794-160000 au 0675-666333. Na hapa ningependa kusisitiza jambo la msingi, jezi hazitauzwa Super Dome, hakutakuwa na biashara hiyo Super Dome pale tutawapa jezi waliolipa Tsh. 250,000.”Alisema Ahmed Ally.

banner

Kuhusu jezi ambazo zinazalishwa na mzalishaji mkuu wa klabu hiyo kampuni ya JayRutty alisema kuwa kwa msimu huu atatoa pea tatu ambazo zitatumika kwa ajili ya ligi kuu ambazo zote hizo zimetengenezwa nchini Italia yalipo makao makuu ya kampuni ya Diadora.

“Msimu huu tuna jezi tatu ambazo zimetengezwa na JayRutty kwa kushirikiana na Diadora. Kwenye jezi kutakuwa na nembo ya JayRutty na Diadora Msimu huu kuanzia kwenye kudesign hadi kutengenezwa kazi yote imefanyika nchini Italia na tayari zimeshaanza kuwasili nchini Tanzania na tarehe 27/08/2025 zitazinduliwa.”Alimalizia kusema.

Bei ya jezi kwa msimu huu zitakua tofauti na misimu iliyopita ambapo kutokana na ubora wa jezi hizo basi hata bei yake nayo imekua juu kulinganisha na misimu kadhaa iliyopita ambapo zilikua zikipatikana kwa elfu 30 mpaka 35 za kitanzania.

“Jezi ya msimu huu hakuna binadamu yeyote ambaye amewahi kuona jezi nzuri kama hii, ni jezi kali vibaya mno, Diadora wenyewe walikuwa hawaamini kama hiyo jezi inakuja Afrika. Wanasimba wenzangu kila mmoja aandae Tsh. 45,000 ya kununua jezi yake.”Alisema Ahmed Ally mbele ya waandishi wa habari.

Akijibu kuhusu changamoto ya upatikanaji wa jezi feki hasa maeneo ya mjini ambapo kumekua na wimbi la jezi ambazo zina kiwango cha chini huku bei yake ikiwa chini,Meneja huyo wa Habari na mawasiliano alisisitiza kuwa “Mwenye mamlaka ya kutangaza pre order ya jezi ya Simba ni Jayrutty Investment East Africa Ltd pekee. Haruhusiwi mtu yeyote kuandikisha wala kuchukua pre order na tayari mchakato umeshaanza na maombi ni mengi mno. Usisubiri izunduliwe maana chelewachelewa utakuta mwana si wako. Dhamana ni mimi hapa, jezi ya mwaka huu ni ya hadhi ya juu mno.”

Kuhusu hafla hiyo ya uzinduzi wa jezi kuwekwa kiingilio kikubwa Ahmed alisema kuwa hilo linatokana na ukweli kuwa tukio hilo ni zaidi ya uzinduzi wa jezi ambapo pia kutakua na mambo mbalimbali ya kimpira.

“Kwenye usiku wetu pale Super Dome kutakuwa na amtukio mengi kama nilivyosema lakini pia tutapata historia ya Simba SC ya mwaka 1979, na tumemchukua gwiji la habari mzee Tido Mhando nini Simba SC ikicheza na Mufulira Wanderers tukafa bao 4-0 Uwanja wa Uhuru tukaenda Zambia tukapindua matokeo tukampiga bao 5-0. Historia hiyo ambayo Tido Mhando ndio alikuwa Baraka Mpenja wa wakati huo mtangazaji wa michezo hiyo kupitia Radio Tanzania. Tutaipata hiyo historia pale ukumbini na tunafanya hivyo ili kuwarithisha nyie vijana wadogo mambo makubwa ambayo Simba Sports club amewahi kuyafanya barani Afrika.” Alimalia kusema Ahmed Ally

Mpaka sasa mashabiki wa klabu hiyo na wafanyabiashara kwa ujumla wanasubiri kwa hamu uzinduzi wa jezi hizo ili waanze kuuza rasmi kwani imekua ni biashara inayolipa ndani ya muda mfupi.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited