Sports Leo

Dube Aipa Matumaini Yanga Sc

Bao la dakika za mwishoni la Prince Mpumelelo Dube dhidi ya Tp Mazembe limerudisha matumaini ya Yanga sc kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika baada ya kupata sare ya 1-1 na kuambulia alama moja katika mchezo huo uliochezwa jijini Lubumbashi.

Yanga sc ikiwa imepoteza michezo yake yote miwili dhidi ya MC Algers na Al Hilal Fc ilihitaji ushindi wa aina yeyote ili kupata alama tatu lakini ilijikuta matatani baada ya kupigwa bao la kichwa na Cheick Fofana dakika ya 42.

Kitendo cha kocha Sead Ramovic kumuanzisha Mudathir Yahaya kama kiungo mshambuliaji kiliwanyima Yanga sc nafasi za kuisogelea Tp Mazembe lakini mabadiliko ya kuwaingiza Stephan Aziz Ki na Prince Dube yaliwalipa Yanga sc baada ya kuanza kushambulia.

Clement Mzize aliingia na kasi iliyowasumbua Tp Mazembe upande wa kushoto hali iliyowapa Yanga sc hali ya kujiamini wakilisogelea lango la Mazembe mara kwa mara na hatimaye dakika za nyongeza baada ya muda wa kawaida kutamatika Prince Dube aliuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Mazembe na kuandika bao la kusawazisha lililorudisha matumaini kwa Yanga sc.

Kutokana na kupata sare hiyo sasa Yanga sc imepata alama moja ikiwa mwishoni mwa kundi A huku Al Hilal Fc ikiwa kileleni na alama tisa na Mc Algers ikiwa katika nafasi ya pili na alama nne huku Mazembe ikiwa katika nafasi ya tatu na alama mbili.

Yanga sc inapaswa kushinda mchezo ujao nyumbani dhidi ya Tp Mazembe ili kuchukua alama tatu na kufikisha nne huku pia iifunge Mc Algers itakapokuja hapa nchini.

Exit mobile version