Site icon Sports Leo

Mabosi Dodoma Jiji Kumjadili Mashamo

MABOSI wa Dodoma Jiji FC wanatarajia kukutana muda wowote kuanzia sasa kuweka mambo sawa juu ya mustakabali wa kocha wao mkuu raia wa Rwanda, Vincent Mashami, ambaye kwa sasa yuko katika hali ya sintofahamu kutokana na sintofahamu ya leseni yake ya ukufunzi.

Mashami, ambaye alichukua mikoba ya Mecky Maxime mwanzoni mwa msimu huu, ameweka timu katika mazingira magumu baada ya klabu hiyo kutozwa faini ya Sh15 milioni na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kutokana na timu hiyo kucheza mechi tatu mfululizo bila kuwa na kocha mkuu aliyekidhi vigezo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, kikao cha viongozi wa juu kinatarajiwa kufanyika haraka iwezekanavyo kujadili namna ya kumsaidia Mashami kutatua tatizo hilo kabla hali haijawa mbaya zaidi. Moja ya ajenda kuu ni kujua kama kuna uwezekano wa kocha huyo kushiriki kozi fupi ya kuboresha leseni yake maarufu kama “refresher course” katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Mashami kwa sasa anamiliki leseni ya ukufunzi ya CAF A, ambayo hata hivyo haimruhusu kusimama kama kocha mkuu katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu. Kanuni mpya zinahitaji kocha mkuu awe na leseni ya UEFA Pro au CAF Pro, jambo ambalo linamweka katika wakati mgumu na klabu katika hatari ya kuendelea kutozwa faini.

“Ni kweli tumeumizwa na faini hizi, zinaathiri bajeti na mipango ya timu. Hatuwezi kuruhusu hali hii iendelee. Tunakutana kama uongozi kuona kama tunaweza kumsaidia kupata kozi hiyo ya refresher ili arudi kazini haraka. Hatujamfikiria kumfuta kazi, bado tuna imani naye,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya klabu hiyo.

Licha ya changamoto hizo, viongozi wa Dodoma Jiji bado wanaonekana kumuamini Mashami kutokana na mbinu zake za kiufundi na namna alivyoanza kazi yake kwa kuleta nidhamu mpya kambini. Wachezaji pia wanaripotiwa kuwa na mahusiano mazuri na kocha huyo, jambo linalowapa mabosi wa timu hiyo msukumo wa kutafuta suluhu badala ya kufikiria kumtimua mapema.

Kwa mujibu wa ratiba, Dodoma Jiji inatarajiwa kucheza mechi kadhaa muhimu wiki zijazo, na iwapo suala la Mashami halitatatuliwa mapema, klabu hiyo inaweza kuendelea kutozwa faini au hata kupokea adhabu nyingine kali zaidi kutoka TPLB.

Hali hiyo imewafanya wadau wa soka kuhoji kama usajili wa kocha huyo ulifanyika kwa kuzingatia vigezo vya kikanuni, ama ulikuwa ni mwendelezo wa maamuzi ya haraka yasiyo na tafsiri sahihi ya mabadiliko ya sheria za leseni za makocha barani Afrika.

Mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuona ni uamuzi gani uongozi wa klabu yao utachukua, huku wengi wao wakitaka suala hili lisitatize morali ya kikosi chao ambacho bado kinapambana kujihakikishia nafasi salama kwenye msimamo wa ligi.

Mpaka sasa, uongozi wa Dodoma Jiji haujatoa tamko rasmi, lakini taarifa za ndani zinaonesha kuwa msimamo wao ni mmoja – kumsaidia Mashami kwa kila njia ili arejee rasmi kuiongoza timu yake ndani ya benchi, bila kuigharimu klabu zaidi kifedha wala kiufundi.

Exit mobile version