Kwa mara nyingine tena, jina la Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji limeibuka kwenye vichwa vya habari vya soka nchini Tanzania. Safari hii si kwa sababu ya Simba SC – timu ambayo amewekeza damu, jasho na fedha kwa miaka mingi – bali kwa uamuzi wake mpya wa kuidhamini klabu ya Coastal Union kupitia bidhaa yake ya sabuni ya Mo Taifa. Hatua hii imeibua mjadala mzito, lakini pia inatoa taswira mpya ya namna soka la Tanzania linavyogeuka kuwa biashara halisi.
Katika hafla maalum iliyofanyika Tanga, Uongozi wa Coastal Union ulitangaza rasmi udhamini huo wa kutoka bidhaa hiyo inayozaliwa na kampuni ya Metl inayomilikiwa na Mo Dewji, Coastal Union kama moja ya klabu kongwe na zenye historia ndefu kwenye soka la Tanzania. Mo ameonyesha kuwa huu ni mwanzo tu wa mkakati mpana wa kuisaidia Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa ligi ya ushindani wa kweli barani Afrika, akiamini kuwa soka ni zaidi ya uwanja – ni uchumi, ajira na burudani.
Uamuzi Uliozua Mjadala
Hata kabla ya wino kukauka, mitandao ya kijamii ililipuka. Mashabiki wa Simba SC – timu inayodhaminiwa na Mo Dewji kama mfadhili mkuu – walionesha sintofahamu. Wengi walihoji: “Inawezekana vipi bilionea mmoja kudhamini klabu zaidi ya moja?” Hali hii iliwakumbusha kelele zilizowahi kutokea kuhusu GSM – mfanyabiashara mkubwa na mfadhili wa Yanga SC – ambaye pia alikuwa anadhamini vilabu vingine kupitia kampuni yake ya GSM.
Lakini kwa jicho la tatu, hatua ya Mo Dewji inaweza kuwa ndio mwelekeo sahihi wa kulipeleka soka la Tanzania mbele. Katika mataifa yaliyoendelea kisoka kama England, Hispania na hata Afrika Kusini, si jambo la ajabu kwa kampuni moja kudhamini vilabu tofauti, mradi tu hakuna mgongano wa maslahi au ukiukwaji wa maadili ya michezo.
Coastal Union Yapata Neema
Kwa upande wa Coastal Union, huu ni mwanzo mpya. Mo Dewji hajaleta tu fedha, bali kaweka imani. Katika kipindi ambacho baadhi ya vilabu vinahangaika kupata jezi, mishahara au hata malazi kwa wachezaji, Coastal Union sasa ina nafasi ya kujipanga vizuri, kufanya usajili wa maana na kupambana vikali kwenye Ligi Kuu ya NBC.
Msemaji wa Coastal Union Hussein Diego alinukuliwa akisema: “Tumepata mdhamini ambaye si tu ana uwezo, bali ana uelewa wa soka. Tunajivunia kuwa sehemu ya familia ya Mo Taifa na taarifa zaidi zitawajia muda si mrefu pindi kila kitu kitakapokua tayari.” Maneno haya yanadhihirisha kuwa Coastal hawajapewa msaada, bali wamepewa fursa ya kufufua ndoto zao za miaka mingi.
Ushindani Waongezeka
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Kama kuna jambo moja ambalo Mo Dewji amelifanya kwa ustadi, ni kuchochea ushindani. Kupitia udhamini huu, anachochea hali ya afya ya soka – timu zote kuwa na uwezo wa kifedha wa kushindana bila kubebwa. Hii inaondoa mawazo ya kwamba ligi hii ni ya timu mbili tu – Simba na Yanga.
Kwa upande mwingine, huu ni ujumbe mzito kwa wafanyabiashara wengine: soka ni jukwaa zuri la kutangaza bidhaa na kuwafikia Watanzania kwa wingi. Mo ameonesha mfano. GSM ameonesha njia. Ni wakati wa wengine kama Bakhresa, Rostam Aziz, na wakubwa wengine kuingia kwenye mchezo huu.
Hisia za Upendeleo? Tuwe na Imani, Vyombo Vyetu Vipo
Ni kawaida kwa mashabiki kuwa na wasiwasi. Katika dunia ya leo ya soka, kila uamuzi wa mdhamini unaweza kuonekana kama “bendera ya tahadhari.” Lakini ili ligi yetu ikue, tunahitaji kuacha siasa za mapenzi ya klabu na kuangalia maslahi mapana ya mchezo wenyewe. Tukianza kushuku kila kitu, basi hakutakuwa na mdhamini atakayeweza kuvumilia kelele za mitandaoni.
Na kama kuna kweli viashiria vya upangaji matokeo, basi taasisi kama TAKUKURU, TFF, na Jeshi la Polisi
zifanye kazi yao kikamilifu. Hili si jambo la mashabiki mitandaoni – ni jukumu la vyombo rasmi vya kusimamia haki na sheria.
Hitimisho: Udhamini Ni Injini Ya Maendeleo
Uamuzi wa Mo Dewji kuidhamini Coastal Union si kosa – ni zawadi. Ni tiketi ya maendeleo kwa klabu hiyo na changamoto kwa vilabu vingine. Kama kweli tunataka ligi bora, basi lazima tukubali ukweli huu: soka la kisasa haliwezi kuendelea bila fedha. Na fedha zinapatikana kwa njia ya udhamini.
Tunahitaji kuona matajiri wengi zaidi wakijitokeza – si kwa sababu ya mapenzi ya klabu fulani tu, bali kwa ajili ya maendeleo ya soka letu. Kadri vilabu vinavyopata udhamini, ndivyo ushindani unavyoongezeka. Na ligi ikiwa na ushindani wa kweli, taifa linanufaika.
Kwa hiyo, badala ya kulalama, tushangilie udhamini – lakini tusahau uangalizi. Mo amefungua ukurasa mpya – tusome vizuri, tusikurupuke.