Kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza amesema wamejiandaa kuwapa furaha mashabiki wao katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC hapo kesho uwanja wa Benjamini Mkapa.
Ntibazonkiza amerejea kikosini akiwa imara baada ya kupona majeraha ya nyonga yaliyomuweka nje kwa takribani miezi miwili.
Nyota huyo aliyewahi kutamba barani Ulaya, amewataka mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi kwani wamejipanga kupambana katika kila mechi ili kujiimarisha kwenye uongozi wa ligi na kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa.
“Namshukuru Mungu, nimerejea nikiwa fiti, ninaamini nitakuwa na kipindi kingine kizuri, mengine yataonekana kwa vitendo uwanjani, kikubwa ni kuwa na afya njema”
“Mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono, tumedhamiria kufanya vizuri katika michezo iliyobaki, tutapambana kwenye kila mchezo, watafurahi” alisema Ntibazonkiza
Kurejea kwa Ntibanzonkiza kumeongeza mzuka kwenye kikosi cha kocha Juma Mwambusi ambaye kesho ataiongoza Yanga katika mchezo wake wa kwanza akikaimu nafasi ya Kocha Mkuu..