Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuchukua alama tatu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini dhidi ya Klabu ya Mashujaa Fc baada ya kuifunga klabu hiyo kwa 5-0 mchezo wa ligi kuu uliofanyika katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Yanga sc imefanikiwa kupata ushindi huo mkubwa ugenini ikiwa ni mara chache sana kushinda idadi hiyo ya mabao ugenini katika michezo ya ligi kuu ya Nbc nchini.
Ikianza na Prince Dube kama mshambuliaji wa kati akisaidiwa na Clement Mzize na Stephan Aziz Ki pamoja na Pacome Zouzoua huku safu ya kiungo ikiwa na Khalid Aucho na Duke Abuya aliyechukua nafasi ya Mudathir Yahaya ambaye hakuwepo uwanjani.
Abuya ndiye aliyefungua akaunti ya mabao kwa Yanga sc dakika ya 31 kwa shuti kali baada ya mabeki wa Mashujaa Fc kujichanganya kuokoa mpira uliokua ukizagaa langoni.
Prince Dube alifunga bao la pili dakika ya 48 ya kipindi cha pili akiruka na kupiga kichwa na kumalizia krosi ya Pacome Zouzoua.
Khalid Aucho alifunga bao la tatu kwa faulo iliyopigwa na Pacome Zouzoua na kufunga bao lake la kwanza msimu huu.
Cletous Chama aliingia kuchukua nafasi ya Stephan Aziz Ki huku Maxi Nzengeli akichukua nafasi ya Prince Dube ambapo Chama alifunga mabao mawili dakika za 74 na 83 akimalizia krosi za Nzengeli na Duke Abuya.
Yanga sc sasa imefikisha alama 55 kileleni mwa msimamo wa ligi kuu huku ikiwa imefunga mabao 55 katika michezo 21 ya ligi kuu huku Mashujaa Fc ikisaliwa na alama 23 katika michezo 21 ya ligi kuu.