Klabu ya Yanga SC imeanza kutathmini uwezekano wa kumrejesha kocha wake wa zamani, Sead Ramovic, kurejea Jangwani kufuatia hali ya sintofahamu ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Roman Folz, ambaye amekuwa akikosolewa kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu katika michezo ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa viongozi wa juu wa Yanga SC hawajaridhishwa na kiwango cha timu ambacho kimeonekana kupungua ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita, licha ya uwepo wa kikosi chenye wachezaji wenye ubora wa hali ya juu. Hali hiyo imesababisha kuibuka kwa mjadala wa ndani kuhusu hatma ya Folz, huku jina la Ramovic likitajwa kuwa miongoni mwa wagombea wanaoweza kuchukua nafasi hiyo.
Sead Ramovic, ambaye aliondoka Yanga mwezi Januari mwaka jana na kuelekea nchini Algeria kujiunga na CR Belouizdad, amekuwa katika wakati mgumu klabuni hapo baada ya kuandamwa na matokeo yasiyoridhisha katika ligi ya nchini humo. Ripoti zinasema kocha huyo kwa sasa yupo chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa uongozi wa Belouizdad, na kuna uwezekano mkubwa wa kuachana naye iwapo mambo hayataimarika hivi karibuni.
Yanga SC inaelezwa inataka kutumia kipindi cha mapumziko ya ligi kupisha michezo ya timu za Taifa kutathmini mustakabali wa benchi la ufundi, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo ya awali na wawakilishi wa Ramovic. Uongozi wa Yanga unaamini kocha huyo anaifahamu vyema klabu, mazingira, na wachezaji wengi waliopo sasa, hivyo anaweza kurejesha falsafa ya ushindani iliyoipa mafanikio makubwa kipindi chake cha kwanza.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Hata hivyo, maamuzi ya mwisho yanatarajiwa kufanyika baada ya tathmini rasmi kufanywa na kamati ya ufundi ya klabu hiyo, huku mashabiki wengi wa Yanga wakiwa na maoni tofauti – wengine wakitaka Folz apewe muda zaidi, na wengine wakihitaji mabadiliko ya haraka ili kurejesha makali ya timu hiyo bingwa watetezi wa Tanzania Bara.