Sports Leo

Yanga Sc Yatangulia Fainali Crdb

Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kufuzu hatua ya fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho la Crdb nchini baada ya kuifunga klabu ya Jkt Tanzania kwa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika jioni ya leo katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Yanga sc iliingia katika mchezo huo ikiwaanzisha washambuliaji wake vinara Prince Dube na Clement Mzize huku Maxi Nzengeli na Stephan Aziz Ki pamoja na Mudathir Yahaya na Duke Abuya wakilinda eneo la kiungo.

Jkt Tanzania walisaidiwa na uimara wa mlinda mlango wake Yakub Selemani aliyekua kikwazo kwa Yanga sc kupata bao mpaka dakika ya 41 shuti kali la Prince Mpumelelo Dube lililomshinda kipa huyo na kujaa wavuni.

Yanga sc walikosa mabao mengi ya wazi kupitia kwa Stephan Aziz Ki,Maxi Nzengeli na Clement Mzize ambao zaidi ya mara moja walishindwa kuweka mpira wavuni.

Mabadiliko ya kipindi cha pili kuwaingiza Pacome Zouzoua na Cletous Chama yaliipa nguvu Yanga sc ambapo wawili hao walisaidia upatikanaji wa bao la pili la dakika ya 90 likifungwa na Mudathir Yahaya akipokea pasi ya Cletous Chama aliyepokea mpira mzuri wa Pacome Zouzoua

Yanga sc sasa wanasubiri mshindi baina ya Simba Sc dhidi ya Singida Black Stars ili kufahamu watakutana na nani katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo.

Exit mobile version