Bondia wa Tanzania Abdallah Pazi maarufu kama Dulla Mbabe amepigwa katika pambano la uzito wa kati lililopewa jina la ‘Kiboko ya Wageni’ usiku wa kuamkia dhidi ya Tshimanga Katompa kutoka Congo.
Katika pambano hilo la raundi 10 lililofanyika katika ukumbi wa TPA Sabasaba Jijini Dar es salaam lilishuhudia Dulla akipigwa kwa pointi katika pambano hilo la kusisimua huku ngumi zikipigwa kwelikweli.
Katompa ambaye ambaye ameshinda mapambano yake yote kwa KO alionekana kumfahamu vizuri mpinzani wake huyo kwani alionekana kutawala vizuri mchezo huo licha ya uwepo wa mashabiki wa Dulla Mbabe ukumbini hapo.
Hili ni pambano la pili mfululizo kwa Dulla kupoteza baada ya lile na mpinzani wake wa jadi Twaha Kiduku huku maswali yakiibuka juu ya nini hatma ya mwanamasumbwi huyo ambaye ameanza kupoteza mvuto kwa wapenzi wa ngumi nchini.