Sports Leo

Bajaber na Camara Kuikosa Mechi Muhimu Dhidi ya Nsingizini Hotspurs

Kikosi cha Simba SC kimeondoka nchini leo kuelekea Eswatini kwa ajili ya mchezo muhimu wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs, huku habari mbaya kwa mashabiki zikitangazwa na Meneja Mkuu wa timu hiyo, Dimitar Pantev, aliyethibitisha kuwa nyota wawili muhimu wa kikosi hicho, Mohammed Bajaber na kipa tegemeo Moussa Camara, hawatakuwa sehemu ya msafara huo kutokana na majeraha.

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka Afrika Mashariki na Kati, inatarajiwa kuchezwa Jumamosi ya Oktoba 19, 2025 katika uwanja wa nyumbani wa Nsingizini Hotspurs huko Eswatini, ikiwa ni hatua ya kwanza katika kibarua kigumu cha Simba kuelekea hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa barani.

Bajaber na Camara Kuikosa Mechi Muhimu Dhidi ya Nsingizini Hotspurs-www.Sportsleo.com

Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo asubuhi, Pantev alisema kuwa majeraha ya Bajaber na Camara yamewashtua na kuwaacha na kazi ya ziada kuhakikisha wanapata mbadala bora wa wachezaji hao wawili.

“Ni pigo kwetu. Bajaber alipata majeraha kwenye mchezo wa kirafiki tulipokuwa kambini na ameshaanza matibabu. Camara naye alipata maumivu katika mchezo dhidi ya Namungo Fc . Madaktari wamependekeza wapumzike na waendelee kupata matibabu Dar es Salaam,” alisema Pantev kwa masikitiko.

Mohammed Bajaber, kiungo mshambuliaji mwenye kasi na uwezo wa kuunganisha safu ya kati na ya ushambuliaji, amekuwa akichukuliwa kama moja ya nyota chipukizi walioleta mvuto mpya kwenye kikosi cha Simba msimu huu. Kuwepo kwake katika mchezo dhidi ya Hotspurs kulitarajiwa kuongeza kasi na ubunifu mbele ya lango la wapinzani.

Kwa upande mwingine, Moussa Camara ni mlinda mlango tegemeo ambaye ameonyesha kiwango bora tangu aanze kuaminiwa na benchi la ufundi. Kukosekana kwake kutalazimu kocha mkuu wa timu hiyo kufanya mabadiliko makubwa langoni, huku mlinda mlango namba mbili Yakud Seleman akipewa jukumu zito la kulinda milango ya Wekundu wa Msimbazi katika mechi ya ugenini.

Hata hivyo, Pantev ameongeza kuwa morali ya timu iko juu na wachezaji waliobaki wako tayari kwa mapambano. Amesisitiza kuwa malengo ya Simba hayajabadilika na kwamba wanaamini wataweza kupata matokeo mazuri wakiwa ugenini kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki mbili zijazo jijini Dar es Salaam.

“Simba ni timu kubwa, tuna kikosi kipana. Tuna imani na kila mchezaji aliye kwenye msafara huu. Tunaenda kupambana, kupata matokeo mazuri, na kurudi kwa kishindo,” aliongeza Pantev.

Simba SC, ambayo imekuwa miongoni mwa vilabu vinavyopeperusha vyema bendera ya Tanzania katika anga ya kimataifa, inajivunia uzoefu mkubwa katika mashindano haya ya CAF na inatarajia kutumia uzoefu huo kuwa silaha dhidi ya wapinzani wao kutoka Eswatini.

Wakati mashabiki wa Simba wakisubiri kwa hamu kuona kikosi chao kikitinga hatua ya makundi kwa msimu mwingine tena, ni dhahiri kuwa pengo la Bajaber na Camara litaacha maswali mengi. Hata hivyo, kwa namna ambavyo Simba imekuwa ikijipanga msimu huu, kuna matumaini kuwa vijana waliopo wataweza kusimama imara na kuendeleza rekodi nzuri ya timu hiyo katika mashindano ya kimataifa.

Simba SC inatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho nchini Eswatini siku moja kabla ya mchezo, ambapo kocha mkuu atatumia fursa hiyo kuweka mikakati ya mwisho na kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake kuelekea mchezo huo muhimu wa hatua ya mtoano.

Exit mobile version