Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David Concar amezitembelea klabu kongwe za soka nchini za Simba sc na Yanga sc kwa lengo la kuzifahamu zaidi pamoja na kukuza uhusiano katika uga wa michezo na nchi yake.
Katika ziara hizo ambazo zilianza yalipo makao makuu ya klabu ya Simba sc Masaki jijini Dar es salaam Balozi huyo alipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya klabu hiyo Salim Abdalah ‘Try Again’ pamoja na Afisa Mtendaji mkuu wa klabu hiyo Iman Kajula sambamba na mjumbe wa bodi Asha Baraka ambapo alitembezwa katika baadhi ya idara za klabu hiyo pamoja na kufahamishwa mipango mbalimbali ya klabu ikiwemo mchakato wa mfumo wa mabadiliko ya uongozi wa klabu hiyo.
Pia baada ya hapo Balozi huyo alipelekwa katika viwanja vya mazoezi vya klabu hiyo vya Mo Simba Arena vilivyopo Boko ambapo alipata wasaa wa kuzungumza na wachezaji na benchi la ufundi la klabu hiyo.

Picha ya pamoja baina ya Balozi wa Uingereza nchini David Concar akiwa na wachezaji na benchi la ufundi la klabu hiyo alipowatembelea mazoezi Bunju.
“Nimevutiwa sana na Simba sc ikiwa tayari ni moja ya klabu kubwa barani Afrika na nimependezwa kiukweli na weledi katika klabu,Uongozi na mpaka viwanja vya mazoezi ambapo nimevutiwa sana hasa na usiriazi niliouna”Alisema Balozi Concar
“Nimekua nikiingalia Simba sc kwa mbali lakini sasa nimefika na kujionea mimi mwenyewe na kushuhudia kuanzia kwa uongozi mpaka viwanja vya mazoezi kiukweli weledi unaonekana hadharani”
Balozi huyo baada ya kumaliza ziara hiyo upande wa Simba sc moja kwa moja alielekea katikati ya jiji eneo la Posta zilipo ofisi za klabu ya Yanga sc katika jengo la Salamanda Tower ambapo alipokelewa na Rais wa klabu hiyo Eng.Hersi Said sambamba na makamu wa Rais Arafat Haji na Afisa Mtendaji mkuu Andre Mtine ambapo pamoja na Utambulisho Balozi huyo alitembezwa katika Idara mbalimbali za klabu hiyo sambamba na kuelezwa namna mchakato wa mabadiliko wa klabu hiyo ulipofikia.
Jioni Balozi Concar alitembelea eneo la Avic Town Kigamboni ilipo kambi ya klabu ya Yanga sc ambapo alikutana na wachezaji sambamba na kujionea namna miundombinu ya mazoezi ya klabu hiyo.
“Katika uga wa mpira wa Afrika Yanga sc ni sehemu muhimu sana hivyo asanteni sana na sasa najua kwanini kauli mbiu yetu ni daima mbele nyuma mwiko”Alisema balozi huyo na kuibua kicheko kwa wachezaji waliokua wanamtazama kwa bashasha.