Home Soka FIFA Yaipokonya Afrika Kusini Alama 3 Kisa Mokoena

FIFA Yaipokonya Afrika Kusini Alama 3 Kisa Mokoena

by Dennis Msotwa
0 comments

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeipokonya timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) alama tatu walizozikusanya katika ushindi wao dhidi ya Lesotho, kufuatia kosa la kumchezesha kiungo Teboho Mokoena ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Mchezo huo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 ulifanyika mwezi Machi 2025, ambapo Afrika Kusini walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Lesotho, kupitia magoli yaliyofungwa na Relebohile Mofokeng dakika ya 60, na Jayden Adams dakika ya 64. Hata hivyo, ushindi huo sasa umebatilishwa baada ya kubainika kuwa Mokoena hakupaswa kushiriki mechi hiyo kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano alizokusanya katika michezo ya awali ya kufuzu.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na FIFA, imethibitishwa kuwa Lesotho wamepewa ushindi wa mabao matatu kwa bila (3-0) kwa mujibu wa sheria za mashindano, huku Afrika Kusini wakipokonywa alama zao zote tatu walizozipata uwanjani. Uamuzi huo umepokelewa kwa mshtuko mkubwa na mashabiki wa Bafana Bafana, ambao walikuwa na matumaini makubwa ya kuona timu yao ikisonga mbele kwenye hatua za kufuzu.

FIFA Yaipokonya Afrika Kusini Alama 3 Kisa Mokoena-Sportsleo.co.tz

Aidha, Shirikisho la Soka la Afrika Kusini (SAFA) limepigwa faini ya Faranga 10,000 za Uswizi, sawa na zaidi ya shilingi milioni 30 za Kitanzania, kwa kosa la uzembe wa kutozingatia kanuni za usajili na uhalali wa wachezaji. FIFA imesisitiza kuwa wajibu wa kuhakikisha mchezaji haruhusiwi kucheza akiwa na adhabu uko mikononi mwa shirikisho husika.

Tukio hili limezua mjadala mkubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, huku wachambuzi wa soka wakikosoa vikali SAFA kwa kushindwa kufuatilia hali ya kadi kwa wachezaji wake. Wengi wanaona kosa hilo kama la kizembe ambalo linaweza kuigharimu sana Afrika Kusini katika mbio za kufuzu Kombe la Dunia.

Kwa sasa, Lesotho wamenufaika moja kwa moja kwa kuongezewa alama tatu na tofauti ya mabao matatu, hali inayowapa nafasi nzuri zaidi katika kundi lao la kufuzu. Wakati huo huo, Bafana Bafana wamelazimika kurudi nyuma katika msimamo wa kundi, na sasa wanakabiliwa na presha kubwa ya kushinda michezo yao iliyobaki ili kufufua matumaini ya kufuzu.

SAFA bado haijatoa tamko rasmi kuhusiana na uamuzi huo wa FIFA, lakini inatarajiwa kufanya kikao cha dharura kuamua hatua za kuchukua, ikiwemo uwezekano wa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited