Home Soka Hemed Morocco Abwanga Majina Makubwa Stars

Hemed Morocco Abwanga Majina Makubwa Stars

by Dennis Msotwa
0 comments

Dar es Salaam, Oktoba 1, 2025 – Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Hemed Suleiman ‘Morocco’, ametangaza kikosi kipya kitakachoingia kambini rasmi Oktoba 4, 2025 kujiandaa na mchezo muhimu wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia, huku akifanya mabadiliko makubwa yaliyowashangaza wengi.

Katika orodha hiyo, Hemed Morocco ameonyesha dhamira ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya kikosi kwa kuwaacha nje baadhi ya wachezaji waliodumu kwa muda mrefu, huku akiwaita nyota wapya waliokuwa nje ya timu hiyo kwa kipindi kirefu.

Wapya Watinga Stars

banner

Majina kadhaa mapya na yaliyosahaulika yamerejea kikosini, miongoni mwao wakiwa ni mabeki wa Yanga SC Israel Mwenda, Aziz Andambwile, na Bakari Mwamnyeto, pamoja na kiungo mwenye kasi na ubunifu Offen Chikola, ambaye amekuwa kwenye kiwango bora ndani ya kikosi hicho cha Jangwani.

Vilevile, Habib Idd wa Singida Black Stars amerudi kundini baada ya muda mrefu, huku kiungo wa kati Morice Abraham wa Simba SC naye akiitwa tena katika kikosi hicho. Lakini pengine jina lililoshangaza wengi ni la Edwin Balua, anayecheza soka la kulipwa nchini Cyprus katika klabu ya Enparalimniou – akirejea baada ya kipindi kirefu cha kutoitwa huku akionyesha maendeleo makubwa barani Ulaya.

Wakongwe Wabwagwa

Katika hali isiyotarajiwa, Hemed Morocco ameacha majina makubwa na maarufu ambayo yamekuwa mhimili wa Taifa Stars kwa miaka mingi. Miongoni mwa walioachwa ni beki wa Simba SC – Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Yanga sc ambao walitarajiwa kupewa nafasi kutokana na uzoefu wao katika mechi za kimataifa.

Viongozi wa safu ya ushambuliaji kama Mbwana Ally Samatta na Simon Msuva, ambao wamekuwa nembo ya Taifa Stars kwa zaidi ya miaka 10, pia hawapo kwenye orodha hiyo, jambo lililozua gumzo mitandaoni huku wengi wakijiuliza iwapo huu ni mwisho wa enzi yao ndani ya timu ya taifa.

Vilevile, mshambuliaji Kelvin John, anayekipiga katika ligi ya daraja la kwanza nchini Sweden, ameendelea kuachwa licha ya kuonyesha kiwango kizuri katika klabu yake.

Nini Kinaendelea?

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF, Hemed Morocco amesisitiza kuwa uchaguzi wa wachezaji umezingatia “kasi, utayari wa kimwili, nidhamu ya kiuchezaji na mahitaji ya kiufundi” kuelekea mchezo dhidi ya Zambia, unaotarajiwa kuwa mgumu na wa ushindani mkali.

Kocha huyo amesema kuwa huu ni wakati wa kutoa nafasi kwa damu mpya na kurejesha ushindani kikosini, ili kuhakikisha Tanzania inasalia kwenye ramani ya soka la kimataifa kwa mafanikio ya kweli.

“Taifa Stars si ya mtu binafsi. Ni timu ya taifa, na kila mchezaji anayestahili atapata nafasi,” alisema Hemed Morocco wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Mashabiki Wagawanyika

Uamuzi wa kuacha baadhi ya mastaa umepokelewa kwa hisia tofauti mitandaoni. Wapo wanaounga mkono mageuzi hayo kwa kusema yamechelewa, huku wengine wakihofia kuwa kuwakosa wakongwe kama Samatta na Msuva kunaweza kudhoofisha uzoefu kwenye mechi ngumu kama dhidi ya Zambia.

Hata hivyo, wengi wanaisubiri kwa hamu mechi hiyo ya kufuzu ili kuona sura mpya zitakavyotumika na kufanikisha ndoto ya Watanzania kuona Taifa Stars ikishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited