Klabu ya Simba sc kupitia kwa meneja wa Idara ya habari ya klabu hiyo Ahmed Ally imetangaza kuwa beki wa klabu hiyo raia wa DR Congo Henock Inonga atakua mgeni rasmi katika mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Janweng Galaxy utakaofanyika siku ya Jumamosi Machi 2 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Inonga amepewa heshima hiyo ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kuifikisha timu yake ya Taifa ya Congo hatua ya nusu fainali ya michuano ya mataifa ya Afrika (Afcon 2023) yaliyomalizika nchini Ivory Coast ambapo beki huyo alicheza zaidi ya asilimia tisini ya michezo hiyo.
“Mgeni rasmi katika mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy ni Henock Inonga sababu ndio mchezaji pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ameifikisha timu yake ya taifa kwenye nafasi ya nne kwenye AFCON 2023.” Alisema Ahmed Ally wakati akizungumza na waandishi wa habari mchana wa leo akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo huo.
Pia Ahmed aligusia kuhusu timu za Tanzania kufuzu hatua ya robo fainali ikiwemo Yanga sc ambayo imefuzu kwa kuifunga Cr Belouzdad kwa mabao 4-0 ambapo alisema kuwa anayepaswa kushukuriwa ni muwekezaji wa klabu hiyo Mohamed Dewji kwa uwekezaji uliotukuka kiasi cha kuwaamsha wawekezaji wengine.