Kocha za zamani wa Azam Fc Joseph Omog ametambulishwa kuwa kocha mkuu wa wakata miwa wa Manungu Morogoro klabu ya soka ya Mtibwa Sugar baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili mpaka 2023.
Mcameroon huyo aliyewahi kuipa ubingwa pekee wa ligi kuu klabu ya Azam Fc mwaka 2013 amerudi kwa mara tatu kuvifundisha vilabu vya Tanzania baada ya Azam na Simba na sasa Mtibwa.
Jukumu kubwa la kocha huyo ni kuirudisha tena Mtibwa kwenye ukubwa na ubora wake baada ya kunusurika kushuka daraja ndani ya misimu miwili mfululizo,lakini pia kuiwezesha klabu hiyo kushiriki tena michuano ya kimataifa kama moja ya malengo ya msimu kutokana na usajili uliofanyika.
Omog amechukua nafasi ya Mrwanda Hitimana aliyewaacha Mtibwa kwenye mataa na kutimkia Msimbazi,na anaenda kuungana na wachezaji wapya na wenye uzoefu kama Said Ndemla,Abdi Banda,Steve Nzigamasabo na Perfect Chikwende waliosajiliwa msimu huu katika klabu hiyo.
Baada ya kutambulishwa kwa waandishi wa habari kocha huyo alienda moja kwa moja kutambulishwa kwa wachezaji na kuanza kazi yake mara moja.
Mtibwa itaanza mchezo wake wa kwanza wa ligi Jumatatu ya Septemba 27 dhidi ya Mbeya Kwanza katika uwanja wa Jamhuri hivyo ana muda mchache kuhakikisha anaiwezesha timu hiyo kupata matokeo katika mchezo wake wa kwanza.