Site icon Sports Leo

Pacome Zouzoua:Kutoka Ligi Kuu Nbc Mpaka Worldcup

Mshambuliaji wa Klabu ya Yanga, Pacome Zouzoua, ameweka historia ya kipekee kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia akiwa bado anacheza ligi hiyo, baada ya kuiwakilisha vyema timu ya taifa ya Ivory Coast katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kenya.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara, jijini Abidjan, Zouzoua aliingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Nicolas Pepe na kutoa mchango wake kwa Tembo wa Afrika waliotawala mchezo kwa asilimia 63 dhidi ya 37 ya Harambee Stars. Ushindi huo umeihakikishia Ivory Coast tiketi ya kwenda Marekani kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Mabao ya Frank Kessie, Yan Diomande na Amad Diallo yaliipa Ivory Coast ushindi muhimu uliowafanya kuhitimisha kampeni ya kufuzu bila kupoteza mchezo hata mmoja. Mabingwa hao wa Afrika wamemaliza wakiwa vinara wa Kundi F kwa pointi 26, wakifuatiwa na Gabon waliokusanya pointi 25. Gambia ilishika nafasi ya tatu kwa pointi 13, huku Kenya ikimaliza nafasi ya nne.

Zouzoua, ambaye hii ilikuwa mechi yake ya pili kuichezea timu ya taifa, alikuwa sehemu ya kikosi kilichotoa kichapo cha mabao 7-0 kwa Shelisheli kwenye mechi iliyopita, akicheza dakika zote 90. Uwepo wake katika kikosi cha Ivory Coast unaonesha namna Ligi Kuu Tanzania Bara inavyokua na kuzaa wachezaji wanaovutia macho ya timu kubwa za kitaifa barani Afrika.

Katika mechi hiyo dhidi ya Kenya, nyota mwingine wa Yanga, Duke Abuya, pia alipata nafasi ya kuingia uwanjani dakika ya 67 kuchukua nafasi ya mshambuliaji matata wa Kenya, Michael Olunga. Hii ni ishara kuwa Ligi ya Tanzania sasa si ya kubezwa tena, kwani inazalisha vipaji vinavyotoa mchango wa moja kwa moja kwa timu za taifa.

Ivory Coast sasa inajiunga na mataifa mengine makubwa barani Afrika yaliyofuzu Kombe la Dunia 2026, yakiwemo Misri, Cape Verde, Tunisia, Morocco, Algeria, Ghana, Afrika Kusini na Senegal. Huku timu nyingine zikisubiri hatima yao kupitia nafasi ya mshindani bora, Tembo hao wameweka wazi dhamira yao ya kwenda Marekani, Canada na Mexico kwa kishindo.

Kombe la Dunia la mwaka 2026 litafanyika katika majiji 16 ya mataifa matatu — Marekani, Canada na Mexico — kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, 2026. Michuano hiyo inatarajiwa kuwa ya aina yake, kutokana na upanuzi wa idadi ya timu hadi 48, ambapo Afrika itawakilishwa na timu 9 zilizoingia moja kwa moja na nyingine kupitia mchujo maalum.

Historia aliyoiandika Zouzoua si tu fahari kwa Yanga, bali pia kwa Ligi Kuu Bara ambayo sasa inazidi kujiweka kwenye ramani ya soka la kimataifa. Ni hatua inayotoa matumaini makubwa kwa vipaji vingine nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwamba ndoto za kucheza kwenye majukwaa makubwa kama Kombe la Dunia zinaweza kufikiwa hata ukiwa kwenye ligi za ndani.

Exit mobile version