Mabingwa wa soka Tanzania Bara klabu ya soka ya Simba imelazimika kuachia jezi mpya zitakazotumika kwaajili ya michuano mbalimbali itayoshiriki timu hiyo kwa msimu wa 2021/2022 baada ya kuvuja kwa jezi hizo.
Awali uzinduzi rasmi wa jezi hizo ulitarajiwa kufanyika kesho Jumamosi Septemba 4 lakini wamelazimika kuziachia jezi hizo hii leo kwa kile wanachodai ni presha kubwa kutoka kwa mashabiki kuzihitaji jezi hizo.
Kaimu Afisa habari wa Simba SC Ezekiel Kamwaga amesema kuwa ”mashabiki wanahitaji sana jezi,uongozi umeona hauwezi tena kusubiri,presha ni kubwa sana.Sasa rasmi jezi za Simba zinapatikana leo kwenye maduka yote ya VUNJABEI.Uzinduzi uko palepale kesho”.
Katika hatua nyingine kuthibitisha kuvuja kwa jezi hizo Kamwaga amesema ”kuna timu kama Coastal Union wametoa jezi lakini hazikuvuja,imefika Simba jezi imevija.Hii ni tabia mbaya,kwanini uvujishe jezi ya timu?tukianza utani wa jadi wa kuvujishana jezi tunapokwenda itakuwa ni vita”.
Simba wameachia jezi za aina nne ambazo ni ya nyumbani(nyekundu),ugenini(nyeupe),ya tatu(nyeusi) na casual.