Historia imeandikwa! Singida Black Stars wamepiga hatua kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwao baada ya kufanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la CAF, wakifanya hivyo kwa staili ya kisasa na kishujaa kabisa.
Katika mchezo uliopigwa usiku wa Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, vijana wa kocha Miguel Gamondi waliwapiga Flambeau du Centre ya Burundi mabao 3–1, ushindi uliowapa jumla ya mabao 4–2 baada ya sare ya awali ugenini. Ilikuwa ni mechi ya aina yake—ya hisia, presha, na historia ikichongwa kwa miguu ya “Walima Alizeti.”
FLAMBEAU WATAKA KUHARIBU SHEREHE
Wageni kutoka Burundi ndio waliokuwa wa kwanza kufungua akaunti ya mabao dakika ya 26, kupitia shuti kali lililomshinda kipa wa Singida. Bao hilo liliwaweka Singida kwenye presha kubwa huku mashabiki wao wakianza kukaa kimya kidogo. Lakini kama ilivyo kwa timu yenye dhamira, vijana wa Gamondi hawakupoteza dira. Waliongeza kasi, wakaanza kumiliki mpira na kusaka bao la kusawazisha kwa ujasiri mkubwa.

WALIMA ALIZETI WAPINDUA MEZA
Kipindi cha pili kilianza kwa moto mkali. Ndipo straika wa DR Congo, Horso Muaku, akaisawazishia Singida dakika ya 54 kwa kichwa kizito kufuatia krosi safi kutoka upande wa kulia wa uwanja. Bao hilo liliibua nguvu mpya kwa mashabiki waliokuwa wamefurika Chamazi wakipeperusha bendera za njano na bluu.
Dakika ya 64, fundi wa Zambia Clatous Chama, maarufu kama Mesi wa Singida, aliandika bao la pili kwa mkwaju wa kiufundi uliompoteza kipa wa Flambeau baada ya beki wa timu hiyo kuunawa mpira akiokoa shuti la Muaku. Uwanja ukalipuka! Mashabiki wakaanza kuimba “Hii ndiyo Singida mpya, hatuogopi mtu!”
Kisha dakika ya 83, beki hatari Idriss Diomande akamaliza kazi kwa kichwa cha mbali lililomkuta kipa akiwa nje ya mstari wake bao safi lililoweka rekodi ya kihistoria na kuwahakikishia Walima Alizeti safari ya makundi.
GAMONDI AFURAHIA, LAKINI ANATOA ONYO
Baada ya kipenga cha mwisho, kocha Miguel Gamondi alikuwa na kila sababu ya kutabasamu, lakini bado akabaki mnyenyekevu. Akizungumza na waandishi wa habari alisema:
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
“Hatukuanza vizuri kipindi cha kwanza, tulicheza kwa wasiwasi. Lakini mabadiliko tuliyofanya kipindi cha pili yalileta uhai. Nimewaambia wachezaji leo mmefanya jambo la kihistoria, mmeipeleka Singida hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.”
Gamondi aliongeza kuwa safari bado ni ndefu “Hii ni changamoto mpya, itaanza Novemba. Tunapaswa kuonesha ushindani zaidi, hatuwezi kuridhika hapa. Tunataka kuandika historia kubwa zaidi kwa klabu hii,” alisema kwa msisitizo.
KOCHA FLAMBEAU AKIRI PRESHA ILIKUA KUBWA
Kwa upande wa Flambeau, kocha Rukundo Jean De Dieu alikiri kuwa vijana wake walishindwa kudhibiti presha“Tulianza vizuri, lakini presha ya ugenini na kelele za mashabiki ziliwachanganya vijana wangu. Wengi wao bado wachanga, hawajazoea mazingira makubwa kama haya,” alisema huku akikiri kuwa Singida walistahili ushindi.
MASHABIKI WASHANGILIA, MKOANI KUNAVUTIKA
Baada ya mechi, mashabiki wa Singida walisherehekea kwa mbwembwe, wengine wakicheza ngoma ya kisambaa huku wengine wakilia kwa furaha. Mitandaoni, wapenzi wa soka walimimina pongezi wakisema: “Hii ni historia ya kweli kutoka mkoa wa Singida hadi Afrika!”
HITIMISHO
Kwa ushindi huo wa 3–1 na wa jumla wa 4–2, Singida Black Stars wameweka jina lao kwenye ramani ya soka la Afrika. Ni safari ya mafanikio ya klabu iliyoanza kwa ndoto, sasa ikitimiza hazina ya matumaini kwa mashabiki wake.
Gamondi na vijana wake wanajua kilichoko mbele si lelemama, lakini kwa ari, nidhamu na ubora waliouonyesha Chamazi, Singida Black Stars wameonesha kuwa wapo Afrika kuja kushindana, si kutazama wengine wakishindana.