Klabu ya Singida Black Stars ya Tanzania imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji Flambeau du Centre katika mchezo wa hatua ya pili ya michuano hiyo uliopigwa kwenye Uwanja wa Prince Louis Rwagasore, jijini Bujumbura.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa na kasi ya aina yake, Singida Black Stars walionyesha uwezo mzuri, hasa katika kipindi cha pili, na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 55 kupitia kwa mchezaji wao tegemeo, Chama, ambaye alimalizia kwa ustadi mpira wa kurushwa uliochezwa haraka na safu ya ulinzi ya Flambeau kushindwa kuudhibiti.
Bao hilo lilizua shangwe kubwa kwa benchi la ufundi la Singida pamoja na mashabiki wachache wa Tanzania waliokuwa wamejitokeza uwanjani kushuhudia pambano hilo muhimu. Hata hivyo, furaha hiyo haikudumu sana baada ya wenyeji Flambeau du Centre kusawazisha dakika tano baadaye, kufuatia makosa ya wazi ya kipa wa Singida, Amas Abasogie, aliyeshindwa kuwasiliana vyema na mabeki wake na kujikuta akiruhusu bao la kusawazisha.
Makosa hayo yaliipa nafasi Flambeau kuingia mchezoni tena na kuongeza presha langoni mwa Singida, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda huku walinzi wa Singida wakifanya kazi ya ziada kuhakikisha hawaruhusu bao la pili.
Licha ya presha kubwa kutoka kwa wenyeji, Singida Black Stars walijitahidi kucheza kwa nidhamu kubwa na kulinda matokeo, huku wakitegemea mashambulizi ya kushtukiza kupitia kwa washambuliaji wao wa pembeni waliokuwa wakisumbua safu ya ulinzi ya Waburundi.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Kocha mkuu wa Singida,Miguel Gamond, alieleza kuridhika na matokeo hayo akisema: “Tulikuwa na mpango wa kupata matokeo mazuri ugenini. Sare hii ni nzuri kwetu. Tulicheza kwa nidhamu, na licha ya makosa kidogo, vijana walijitahidi. Tunakwenda nyumbani tukiwa na faida ya bao la ugenini.”
Kwa upande wao, mashabiki wa Flambeau du Centre walionekana kutoridhishwa na matokeo hayo, wakielekeza lawama kwa washambuliaji wao waliopoteza nafasi kadhaa muhimu ambazo zingewawezesha kutoka kifua mbele kabla ya kuelekea kwenye mchezo wa marudiano.
Sasa Singida Black Stars wanarejea nyumbani kujiandaa kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa Oktoba 25 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam. Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa aina yake, huku Singida wakiwa na kazi ya kuhakikisha wanamalizia kile walichokianza Bujumbura ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Tayari maandalizi kwa mchezo huo wa marudiano yameanza, na klabu hiyo imewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu yao katika jitihada za kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa.