Klabu ya Yanga SC imeendelea kung’ara barani Afrika baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Weliete Benguela FC ya Angola katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa ugenini. Ushindi huu si wa kawaida tu, bali ni ujumbe mzito kwa wapinzani wa Yanga na pia kwa mashabiki waliokuwa wakihisi shaka juu ya uwezo wa kocha mpya, Romain Folz.
Mabao ya Azizi Andabwile dakika ya 31 kwa shuti kali nje ya mita 18 na lile la Edmund John aliyefunga dakika ya 71 akipokea pasi ya Maxi Nzegeli na bao la Prince Mpumelelo Dube dakika ya 79 akipokea pasi ya Celestine Ecua yalitosha kuipatia Yanga sc ushindi huo muhimu katika mchezo wa awali.
Tangu atue Yanga SC, Folz ameshinda michezo minne mfululizo, na jambo hili linamtengenezea heshima mpya ndani ya klabu na kwa mashabiki. Alianza kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, akafuata kwa ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Bandari FC ya Kenya, kisha akawaumiza mahasimu wakubwa Simba SC kwa bao 1-0, na sasa ameimaliza Weliete kwa mabao 3-0. Hii ni rekodi safi kwa kocha ambaye alipoanza alitazamwa kwa jicho la mashaka.
Moja ya vitu vinavyomtofautisha Folz ni uongozi wake wa kiufundi na mbinu za mabadiliko ya wachezaji. Tofauti na makocha wengi wanaopenda kushikilia kikosi kilekile kila mchezo, Folz anaonekana kupima wapinzani na kuamua nani anafaa kuanza kulingana na hali ya mchezo husika. Kwa mfano, alipoivaa Simba SC, alihakikisha anatumia mfumo imara wa ulinzi na kiungo akiwatumia zaidi Dickson Job na Ibrahim Hamad wakisaidiwa na Aziz Andabwile huku akijikita zaidi kwenye nidhamu ya kiufundi. Lakini alipoivaa Weliete, alifungua mashambulizi kupitia viungo wabunifu na washambuliaji wenye kasi akianza na Clement Mzize na Mohamed Doumbia jambo lililozaa ushindi mnono.
Kitaalamu, ushindi huu mfululizo wa Yanga chini ya Folz unatoa picha kadhaa kwa mashabiki na wachambuzi wa soka:
-
Kurejea kwa kujiamini – Mashabiki waliokuwa wakimtilia shaka sasa wanaanza kuona picha ya kocha anayeijenga timu kwa mfumo thabiti. Kuibuka na ushindi mara nne mfululizo, na zaidi dhidi ya wapinzani tofauti na mazingira tofauti, ni ishara kwamba Yanga ipo kwenye mikono salama.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
-
Nguvu ya wachezaji wote – Folz anatumia kikosi kizima bila kumuacha mchezaji akihisi ametupwa benchi bila nafasi. Hii inaleta ushindani wa ndani ya timu, na kila mchezaji anapopata nafasi yake anajua anatakiwa kutoa asilimia mia moja katika mechi ya derby dhidi ya Simba Sc alianza na Aziz Andabwile ambaye wengi hawakuamini kama anaweza kucheza vizuri na leo kafunga bao huku akiwaacha Mudathir Yahaya na Maxi Nzengeli nje.
-
Mashindano ya Afrika siyo mzaha – Kushinda ugenini kwa mabao 3-0 ni taarifa kubwa. Yanga inajitangaza kuwa si timu ya kubahatisha bali ni klabu yenye mikakati, inayoweza kusafiri popote na kupata matokeo.
-
Uhusiano na mashabiki – Kwa sasa Folz anaanza kujenga imani mpya kwa mashabiki. Wale waliokuwa wakijiuliza kama kweli ana uwezo wa kuiongoza Yanga katika michuano mikubwa sasa wanapata majibu kupitia matokeo haya. Ushindi dhidi ya Simba SC ulikuwa wa heshima, lakini huu wa Weliete ni uthibitisho kwamba Yanga inaweza kupambana Afrika.
Kwa ujumla, Romain Folz anaonekana kujipata katika kazi yake ndani ya Yanga SC. Ushindi huu wa 3-0 dhidi ya Weliete ni zaidi ya alama tatu – ni ishara ya mwanzo mpya, ishara ya matumaini, na ishara kwamba Yanga iko tayari kwa changamoto kubwa za Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa mashabiki wa Yanga, hii ni sababu ya kuondoa shaka na kuanza kuamini kwamba kocha huyu kijana anaweza kuwa chachu ya mafanikio makubwa.