Home Soka Romain Folz: Kocha Kijana Wa Yanga Sc Anayetafuta Muunganiko Katika Kilele Cha Matarajio

Romain Folz: Kocha Kijana Wa Yanga Sc Anayetafuta Muunganiko Katika Kilele Cha Matarajio

by Dennis Msotwa
0 comments

Katika uwanja wa soka wa Tanzania, jina la Romain Folz limeibuka kwa kasi ndani ya klabu ya Yanga SC, baada ya kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyehamia Ismailia ya Misri. Kocha huyu mwenye umri wa miaka 35 tu, amewasili kwa matarajio makubwa, huku akiwa amebeba matumaini ya mashabiki wa Wananchi wanaotamani kuona timu yao ikiendeleza makali ya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Folz si mgeni kwenye soka la Afrika. Akiwa amewahi kuifundisha AmaZulu ya Afrika Kusini, pamoja na timu za Benchem United,Ashanti Gold,Township Rollers na zingine kama kocha mkuu kwa kipindi kifupi, kocha huyu anakuja Yanga akiwa na wasifu wa mbinu mpya, nidhamu na falsafa ya kisasa ya soka.

Msimu huu wa 2025/26, ni yeye ndiye amekabidhiwa jukumu zito la kuhakikisha Yanga inasalia kileleni — si tu katika Ligi Kuu, bali pia katika mashindano ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) ambayo klabu hiyo inashiriki msimu huu ikiwa na lengo la kufika walau nusu fainali.

banner

Tangu aingie kazini, Folz ameiongoza Yanga kupata ushindi katika michezo yote aliyosimama kama kocha mkuu. Timu imeanza vyema kwa kuilaza Rayon Sports ya Rwanda 3-1 katika mchezo wa kirafiki kisha kuibuka na ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Bandari ya Kenya siku ya kilele cha wiki ya mwananchi. Katika michuano ya CAF, Yanga ilionesha ukomavu kwa kuifunga Wiliete ya Angola kwa mabao 3-0, na kufuatiwa na ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, licha ya rekodi hiyo nzuri, baadhi ya mashabiki wameanza kuonyesha dalili za wasiwasi. Wanaona kama vile mbinu za Folz hazijakolea sawasawa, huku wakihisi kuwa bado hajaleta aina ya soka ya “kupendeza macho” ambayo wamezoea kuiona chini ya makocha waliopita kama Nasreddine Nabi,Miguel Gamondi na Miloud Hamdi. Maoni haya si ajabu — soka la Tanzania limekua kwa haraka, na mashabiki sasa wanataka si tu ushindi, bali pia burudani uwanjani.

Lakini hapa ndipo panapohitaji uvumilivu. Ni muhimu kuelewa kuwa kocha Folz yupo katika harakati za kutafuta muunganiko bora wa kikosi, akijaribu mbinu tofauti na kuwapa nafasi wachezaji wote kuonyesha uwezo wao. Katika kipindi hiki, tumeona rotations za kuvutia ambazo zimewafanya wachezaji waliokuwa pembezoni kama Bakari Mwamnyeto na Azizi Andabwile kurejea kwenye kikosi cha kwanza — jambo ambalo linaashiria ushindani mzuri ndani ya timu.

Zaidi ya hayo, Folz ameonesha kuwa hana ubaguzi kwa majina makubwa; anaamini kwenye uwezo wa mchezaji kwa wakati husika, na hilo ni jambo ambalo linaweza kuijenga Yanga kwa upana zaidi kwa mfano kitendo cha kumuanzisha benchi mara kadhaa Moussa Balla Conte. Kwa kufanya hivyo, anajenga msingi imara wa timu yenye kina cha wachezaji, jambo ambalo litakuwa muhimu zaidi msimu utakavyoendelea na ratiba kuwa ngumu.

Mashabiki wa Yanga SC wanapaswa kumtia moyo kocha wao kijana, kwani mafanikio ya kweli hayaji kwa haraka. Mabadiliko ya kiufundi na kimfumo yanahitaji muda, mazoezi, na uaminifu wa pande zote. Romain Folz tayari ameonyesha dalili za kuwa na dira, nidhamu na uthubutu wa kufanya maamuzi magumu — sifa muhimu kwa kocha anayetaka kuandika historia.

Kwa sasa, Yanga inashinda, haijafungwa, na inaonyesha ubora wa kiufundi unaoimarika siku hadi siku. Ni wakati wa kuunga mkono, si kukosoa bila kujenga. Wananchi, vumilieni, muamini mchakato, na mjue kuwa mwanga upo mbele, kama Folz ataendelea kuungwa mkono.

Mwisho wa siku, si kila mafanikio huja kwa kishindo — mengine hujengwa kimya kimya, mazoezini, na kwa subira.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited