Timu ya Arusha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kupitia Ofisa habari wake Bahati Msilu wameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuta msimu wa Ligi Daraja la Kwanza 2019/20 kutokana na janga la Virusi vya Corona linaloendelea kuitikisa Dunia.
Msilu alisema hayo baada ya kuona mapumziko ya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 yameharibia utaratibu wote kwa kusababishia gharama zisizokuwa za lazima kwani wametumia gharama ambazo hawakupaswa kutumia kulingana na hali mbaya ya kiuchumi ya timu.
“ TFF kwa msimu huu wa 2019/20 wangeacha tujiandae kwa msimu ujao, ligi ikiendelea ushindani utakuwa mdogo kwakuwa wachezaji wengi hawana nidhamu ya kufanya mazoezi watarudi wakiwa wazito ukichanganya na janga la Covid-19 hali ya uchumi imekuwa ngumu” , alisema Msilu
Aliongeza kwa kusema kama TFF wataruhusu ligi iendelee basi watoe walau wiki mbili za kujipanga kila mchezo kutokana na hali mbaya kiuchumi.