Klabu ya Coastal Union yenye makao yake jijini Tanga inapiga hesabu kali za kumchukua aliyekuwa kocha wa Tabora United Anicet Kiazayidi kushika nafasi ya Joseph Lazaro msimu ujao.
Wagosi wa kaya wanaona kama kocha huyo raia wa Congo Drc ni mrithi sahihi wa Juma Mwambusi aliyeondolewa kutokana na matokeo mabaya ambayo klabu hiyo ilikuwa ikiyapata.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya klabu hiyo ambacho kiliweka wazi mipango ya klabu hiyo ya kumchukua Anicet kutokana na uwezo aliouonyesha alipokuwa Tabora kabla ya kwenda mafunzoni na kuachana na klabu hiyo.
“Coastal inaamini kuwa, ikimpata Anicet timu hiyo inaweza kurejea kwenye ubora wake wa msimu uliopita, kutokana na kile ambacho wamekiona kwa Tabora United. Ni kocha mzuri kweli hivyo kama mabosi watafikia makubaliano, basi tutakuwa naye na mtamuona ila kwa sasa jina lake ndilo lililopo vichwani mwa matajiri hao wa Tanga,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo Coastal itakua na kazi rahisi ya kumshawishi kocha huyo kutokana na ukweli kwamba kwa sasa hana timu tangu alipoachana na Tabora United ambapo ilisemekana kuwa alikosana na mabosi wa juu wa klabu hiyo.
Coastal Union ambayo msimu uliomalizika ilikuwa nafasi ya nne na ikafanikiwa kushiriki michuano ya CAF, sasa iko namba 10 katika msimamo ikiwa na pointi 31 ikishinda mechi saba, sare 10 na kupoteza 11.