Home Makala ELIE MPANZU: SILAHA MPYA YA SIMBA SC KUELEKEA LIGI KUU NA MICHUANO YA CAF

ELIE MPANZU: SILAHA MPYA YA SIMBA SC KUELEKEA LIGI KUU NA MICHUANO YA CAF

by Dennis Msotwa
0 comments

Klabu ya Simba Sc imekuwa ikifanya usajili wa kishindo kila msimu, lakini ujio wa kiungo mshambuliaji Elie Mpanzu aliyetua klabuni hapo dirisha dogo msimu uliopita umetazamwa kama suluhisho la changamoto za kiufundi zilizokuwa zikiiandama timu hiyo msimu uliopita.

Mashabiki wa Msimbazi sasa wana kila sababu ya kutabasamu, kwani staa huyu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amekua moto wa kuotea mbali, ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa namna anavyowahenyesha mabeki wa timu pinzani.

Mpanzu aliingia Simba sc katika kipindi ambacho timu hiyo ilikua inahitaji kuboresha ubora wake wa kiufundi, hususan eneo la kati na safu ya ushambuliaji ambapo Msimu uliopita, Simba ilionekana kuhitaji kiungo mwenye uwezo wa kusoma mchezo, kushambulia kwa kasi, na kusambaza pasi sahihi kwa washambuliaji wake na hapo ndipo jina la Mpanzu linapopata maana kubwa kwani ni mchezaji mwenye uwezo wa kupenya katikati ya wapinzani na kutoa pasi za mwisho zenye madhara.

banner

Nguvu yake kikosini

Mpanzu ni kiungo anayeweza kucheza nafasi ya namba 8 au 10, akiwa na uwezo wa kuchanganya soka la nguvu na ubunifu. Ana stamina ya hali ya juu, nidhamu ya kiuchezaji na ufundi wa kisasa. Hii inamaanisha namna Simba Sc imekua na urahisi wa kumiliki mpira katikati, huku ikipunguza mashambulizi ya wapinzani. Aidha, uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali umekua silaha nyingine ya kutisha kwa wapinzani wa ligi kuu ya NBC.

ELIE MPANZU: SILAHA MPYA YA SIMBA SC KUELEKEA LIGI KUU NA MICHUANO YA CAF-sportsleo.co.tz

Ndoto ya Simba Afrika

Simba SC haina siri kuhusu malengo yake barani Afrika kuwa ni kutamba tena katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mpaka kuchukua kombe hilo muhimu na kubwa kwa ngazi ya vilabu na katika safari hiyo, mchango wa Mpanzu utakuwa muhimu zaidi.

Katika mechi ngumu dhidi ya vigogo wa Afrika Kaskazini kama Al Ahly, Esperance au Wydad, Simba inahitaji kiungo mwenye uwezo wa kushindana kimwili na kiufundi vitu ambavyo vyote vinapatikana kwa Mpanzu kwani ana uzoefu wa kucheza mpira wa kasi na presha kubwa, jambo linalomfanya kuwa nyota atakayebeba matumaini ya mashabiki katika safari ya kimataifa.

Uhusiano na wachezaji wenzake

Kikosi cha Simba kina nyota wengi wa kimataifa, akiwemo Rushine De Reuck, Jean Charles Ahoua na  Steven Desse Mukwala pamoja na Jonathan Sowah ambapo  mchanganyiko huu ukichanganywa na ubunifu wa Mpanzu, unaunda mstari wa kati na ushambuliaji unaoweza kutengeneza na kutumia nafasi nyingi za mabao.

 

Hii ni ishara kwamba Simba inaweza kurudi kwenye ubora wake wa kufunga magoli mengi, jambo linalovutia mashabiki wake waliotaka kuona timu yao ikifanya maajabu tena hasa baada ya kukaa takribani miaka mitano sasa bila taji la ligi kuu.

Mashabiki wanavyomtazama

Mashabiki wa Simba tayari wamempokea Mpanzu kama mkombozi wa eneo la kati. Mitandaoni, wanasema “Mpanzu ndiye injini ya Simba mpya.” Wengine wanaamini kuwa ujio wake ni sawa na kuandika ukurasa mpya wa historia ya Msimbazi. Kila shabiki anasubiri kuona namna atakavyoshirikiana na mastaa waliopo wapya ili kuhakikisha taji la Ligi Kuu linarejea Msimbazi na kikosi kinatinga hatua za juu za CAF Champions League.

 

Kwa ujumla, Elie Mpanzu si tu usajili wa kawaida, bali ni nyota anayetegemewa kuibeba Simba SC msimu wa 2025/26. Kile kinachotarajiwa kwake si maneno matupu bali ni vitendo vitakavyoamua mustakabali wa mafanikio ya Wekundu wa Msimbazi.

Mashabiki wameshajipanga, wanasubiri midundo ya ngoma za Msimbazi zikilia kwa nguvu pale Simba ikipata ushindi huku Mpanzu akiwa injini ya kikosi hicho mbele ya mastaa kama Sowah na Mukwala pamoja na kiungo Jean Charles Ahoua.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited