Home Makala FEISAL SALUM:Mzawa Ghali Zaidi Ligi ya Nbc

FEISAL SALUM:Mzawa Ghali Zaidi Ligi ya Nbc

by Dennis Msotwa
0 comments

Kama ulikuwa bado hujui kuwa soka la Tanzania linakua kwa kasi, basi hebu mtazame Feisal Salum “Fei Toto” Kiungo fundi wa Azam FC sasa amekuwa mchezaji anayelipwa zaidi kwa wachezaji wazawa nchini, baada ya kusaini mkataba mpya unaomuweka Chamazi hadi mwaka 2027 huku akipokea mamilioni ya shilingi kwa mwezi na zawadi ya kifahari ya gari aina ya Harrier Anaconda.

Katika mkataba huo mpya wa  mwaka mmoja zaidi  ambao sasa utamuweka Chamazi mpaka mwaka 2027 Feisal ameingia rasmi kwenye orodha ya mastaa wa “daraja la kifalme” ndani ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, Feisal sasa atakuwa akilipwa shilingi milioni 50 kwa mwezi baada ya makato, kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa na mchezaji mzawa hadi sasa.

Milioni 500 Dau la Kusainia

banner

Licha ya mshahara wake mkubwa, mkataba huo mpya pia umemletea bonasi ya kusaini (signing fee) ya zaidi ya shilingi milioni 500, fedha iliyolipwa mara moja. Chanzo kutoka ndani ya klabu ya Azam FC kimethibitisha kuwa Feisal alipokea fedha hizo saa chache tu baada ya kuweka saini yake kwenye karatasi ya mkataba mpya.

Mbali na pesa, kiungo huyo pia amepewa gari jipya lenye thamani ya juu, likiwa sehemu ya “good package” ya kumshawishi abakie Chamazi licha ya kuvutia ofa kutoka klabu kadhaa hasa kutoka Yanga sc na Simba Sc pamoja na timu kadhaa za nje ya nchi.

FEISAL SALUM:Mzawa Ghari Zaidi Ligi ya Nbc-sportsleo.co.tz

Msimamo Kama Jiwe,Kuamua Kusalia Chamazi

Wakati mashabiki wengi wa Yanga SC walitamani kumuona Feisal akirudi Jangwani huku pia ikiwa hivyo kwa mashabiki wa Simba Sc wakitamani kuwa na staa huyo, au wengine wakitamani aende Misri, Morocco au hata Qatar, kiungo huyo ametuliza presha zote kwa kuonesha kuwa anaiheshimu Azam FC na ana ndoto ya kuipa mataji makubwa kwa kuamua kusalia huku pia ikielezwa kuwa kocha Florent Ibenge amechangia kwa kiasi kikubwa kumshawishi staa huyo kusalia klabuni hapo.

“Tayari tumefanikiwa kumuongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja zaidi kusalia Azam Fc ambapo sasa atakuwepo mpaka mwaka 2027 na pengine ndie mchezaji anayelipwa zaidi kwa wazawa hapa nchini kwa sasa”Alisema Abdulkarim Amin ambaye ni mtendaji mkuu wa klabu ya Azam Fc.

Feisal Sio wa Kawaida Kawaida

Tangu ajiunge na Azam FC, Feisal amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha timu hiyo, akitoa pasi za mwisho, kusaidia ulinzi, na kutawala eneo la kiungo kwa umahiri wa hali ya juu. Kwa sasa, anachukuliwa kama mmoja wa viungo bora zaidi Afrika Mashariki, na bila shaka ni hazina ya Taifa Stars.

Msimu wake wa kwanza klabuni hapo alifanikiwa kufunga mabao 19 katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huo na kusaidia upatikanaji wa mabao mengine 7 na kufanya jumla kuwa na mchango wa mabao 26 kwa msimu huo ambapo katika msimu wa 2024-2025 pia alitoa asisti 13 akiwa miongoni mwa mastaa waliotoa asisti nyingi zaidi huku akifunga mabao tisa.

Kocha wa Azam FC, raia wa Congo DR Florent Ibenge, amemtaja Feisal kama “mchezaji wa kiwango cha kimataifa ambaye anaweza kucheza ligi yoyote barani Ulaya.

Neema kwa Wazawa Sasa

Hatua ya Feisal kupewa mkataba wa mamilioni imekuwa gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku wachambuzi wa soka wakisema kuwa huu ni wakati wa wachezaji wazawa kuthaminiwa na kulipwa kama walivyo wageni. Wengi wanaamini kuwa mfano wa Feisal unaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye tasnia ya soka nchini.

Tayari Clement Mzize naye amefuata mkondo huo ambao kwa sasa atakua akipokea zaidi ya shilingi milioni 40 za kitanzania ambapo Yanga sc wamefanya maboresho hayo ili mshambuliaji huyo asalia klabuni hapo kumalizia mkataba wake wa miaka miwili iliyosalia wakitegemea atawasaidia katika michuano ya kimataifa msimu huu kabla ya kumuuza msimu ujao.

MWAKA WA FEISAL KUWAKA MOTO?

Kwa mkataba huu mpya na mzigo mzito wa mamilioni mgongoni, matarajio kwa Feisal ni makubwa. Mashabiki wa Azam wanatarajia kumuona akiibeba timu msimu huu kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, FA Cup na hata mashindano ya kimataifa.

Kwa sasa, mzawa huyo wa visiwani Zanzibar si tu mchezaji wa kawaida – bali ni alama ya mafanikio kwa wachezaji wa nyumbani wanaojituma na kuweka juhudi kwenye kazi yao.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited