Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Klabu ya Yanga sc Ally Kamwe anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Tabora kwa makosa ya kutoa maneno ya udhalilishaji dhidi ya Mamlaka za mkoa huo.
Kamwe anatuhumiwa kutoa maneno ya kejeli dhidi ya mkuu wa mkoa wa Tabora Mh.Paul Chacha kuelekea mchezo wa ligi baina ya Yanga sc dhidi ya Tabora United ambapo Yanga sc iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
“Ni kweli tunamshikilia Ali Kamwe ambaye ni Msemaji wa Klabu ya Yanga na tunamfanyia mahojiano kwa tuhuma za kutoa maneno machafu kwa Viongozi wa Serikali na tutatoa taarifa rasmi baada ya mahojiano kukamilika”,Alisema RPC Richard Abwao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora.
Msemaji huyo licha ya kusalimiana kwa bashasha wakati wa mchezo huo na mkuu huyo wa mkoa alikamatwa usiku wa kuamkia leo na mpaka sasa bado anashikiliwa na jeshi hilo.