Home Makala Mayele Mpya Jangwani: Celestine Ecua Aanza Kwa Kishindo Yanga Sc

Mayele Mpya Jangwani: Celestine Ecua Aanza Kwa Kishindo Yanga Sc

Mashabiki Wamuita "Duduwasha"

by Dennis Msotwa
0 comments

Kama hujamsikia Celestine Ecua, basi ujue unachelewa. Ni kama wimbo mpya wenye midundo ya kuvutia ambao umeanza kutikisa anga la soka nchini. Straika huyu hatari kutoka Ivory Coast, amejiunga na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Bara, Yanga SC, akitokea klabu kongwe ya ASEC Mimosas ya kwao Abidjan, na kwa haraka kabisa ameanza kuwapa mashabiki wa Wananchi sababu ya kutabasamu.

Katika michezo mitatu tu aliyocheza hadi sasa – dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, Bandari FC ya Kenya  katika tamasha la Siku ya Wananchi na Simba SC – Ecua amewashangaza wengi kwa kiwango chake cha juu, kasi, ujanja na uwezo wa kumalizia. Hali hiyo imewafanya mashabiki wa Yanga kumwita jina jipya lenye heshima kubwa mitaani: Duduwasha – jina linalomaanisha mchezaji wa kutisha, asiyezuilika.

Mayele Mpya Jangwani: Celestine Ecua Aanza Kwa Kishindo Yanga Sc-sportsleo.co.tz

banner

Mayele Mpya Kwenye Safu ya Ushambuliaji Yanga Sc

Safu ya ushambuliaji ya Yanga SC kwa misimu kadhaa imekuwa ikihitaji mchezaji mwenye mchanganyiko wa nguvu, akili, na uwezo wa kufunga mabao kwa ufanisi mkubwa kama ilivyokua kwa Fiston Kalala Mayele. Hili ndilo linalomfanya Ecua kuwa bidhaa adimu. Katika mchezo dhidi ya Rayon, Ecua alionesha mng’ao kwa kuwasumbua mabeki kwa pressing ya hali ya juu, huku akitengeneza nafasi za mabao ambazo kwa bahati mbaya washambuliaji wenzake hawakuzitumia ipasavyo.

Mchezo wa pili dhidi ya Bandari FC, Ecua alidhihirisha kwa mara nyingine kwamba si mchezaji wa kawaida. Aliweza kufunga bao safi baada ya kumzidi maarifa beki wa kati na kisha kumchambua kipa kama vile anacheza na kijana wa mtaani Kariakoo. Bao hilo liliwafanya mashabiki wa Yanga kupiga mayowe ya furaha, wakiona tumaini jipya mbele ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Derby ya Kariakoo Ilithibitisha Hadhi Yake

Lakini mechi iliyothibitisha thamani halisi ya Ecua ni ile ya watani wa jadi – dhidi ya Simba SC. Licha ya kuwa ni mechi yake ya kwanza ya Derby, presha, upinzani na hadhi ya mchezo huo ni sawa na fainali. Ecua alicheza kwa kujiamini, akionyesha ukomavu wa hali ya juu. Aliwazungusha mabeki wa Simba hasa Rushine De Reuck kama wapo kwenye mazoezi, akatoa pasi ya mwisho ambayo iliokolewa na mabeki hao huku akipiga vibasikeli na chenga kali kwa mwendo wa kasi – tukio lililomwinua kila shabiki aliyekuwepo uwanjani.

Mashabiki wa Yanga waliokuwa na wasiwasi kuhusu nani atakayefaa kuvaa viatu vya washambuliaji waliotangulia kama Stephane Aziz Ki na Fiston Mayele, sasa wanaamini wamepata mtu sahihi. Kila anapogusa mpira, ni kama kuna kitu kinazinduka – mashabiki wanasimama, kelele zinapanda, na jina lake linaitwa kwa sauti kubwa: “Duduwasha! Duduwasha!”

Mchango Wake Kwa Yanga Sc

Celestine Ecua si mfungaji tu. Ni mchezaji anayeweza kucheza kama namba 9 ya kati au akasogea pembeni kama winga. Ana uwezo wa kukokota mpira kutoka katikati ya uwanja hadi kwenye eneo la hatari kwa kasi ya ajabu. Pia ana macho ya kuona pasi, jambo linalomwezesha kushirikiana vyema na viungo kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya.

Kwa mwenendo huu, Yanga SC imepata silaha mpya ya kuogopwa – si tu kwa Tanzania, bali hata kwenye michuano ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika. Kocha Roman Folz sasa anaweza kulala kwa amani, akijua kuwa amepata mchezaji ambaye si wa kusubiri kufunga tu, bali anayeweza kubadilisha matokeo ndani ya dakika chache.

Tuupe Muda Nafasi

Ni mapema mno kumpa sifa zote Celestine Ecua, lakini dalili za mvua ni mawingu. Katika michezo mitatu tu, tayari ameonyesha thamani yake. Kasi, nguvu, maarifa na utulivu mbele ya lango ni mambo yanayomtofautisha na washambuliaji wengi waliowahi kuvalia jezi ya kijani na njano.

Kama ataendelea na kiwango hiki, basi mashabiki wa Wananchi wajiandae kwa msimu wa kushuhudia ‘duduwasha’ wa kweli akitawala vichwa vya habari. Na kwa wapinzani – tahadhari mapema: Mtaani Jangwani kuna mnyama mpya, anaitwa Celestine Ecua – Duduwasha wa Yanga SC!

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited