Kocha Juma Mwambusi ameachana na klabu ya Coastal Union kwa makubaliano ya pande mbili baada ya timu hiyo kuwa na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha katika ligi kuu ya Nbc nchini.
Mwambusi alijiunga na Coastal Union wakati wa dirisha dogo la usajili ambapo alitarajiwa kuleta mabadiliko katika timu hicho baada ya kuchukua nafasi ya David Ouma aliyejiunga na Singida Black Stars.
Kocha huyo amedumu kikosini humo kwa miezi mitano na nusu ambapo pia inatajwa maelewano mabaya na baadhi ya wachezaji kikosini humo kuwa ni moja ya sababu ya kocha huyo kupigwa chini.
“Sio tetesi ni kweli nimeondoka Coastal Union na kuanzia leo hutoniona katika benchi katika mechi na Yanga Sc”.
“Nimeijenga timu, lakini katika ushambuliaji kukawa na tatizo, hali hii imefanya tukose mtililiko wa matokeo mazuri. Hakuna mgogoro katika benchi wala sijagombana na mwenzangu pale benchi, binafsi napenda kusimamia misingi ya kazi yangu”,Alimalizia kusema Mwambusi.
Mpaka anaondoka kikosini humo,Kocha huyo anaiacha Coastal Union katika nafasi ya 13 ya msimamo wa ligi kuu ikiwa na alama 25 katika michezo 25.