Baada ya yule beki katili aliyesajiliwa hivi karibuni na klabu ya Yanga sc Mamadou Doumbia kuishia kukalia benchi na kuwaacha Dickson Job na Yannick Bangala wakijinafasi katika nafasi ya beki za kati za klabu hiyo baadhi ya wadau wa soka wameanza kuhoji kuhusu usajili wa beki huyo.
Doumbia ambaye alisajiliwa kuja kumaliza utata eneo la beki wa kati ambapo ilipaswa Yannick Bangala arudi kucheza eneo la kiungo lakini tangu asajiliwe ameishia kukaa benchi huku katika mchezo dhidi ya Us Monastry timu hiyo ikifungwa mabao ya vichwa mawili ambapo kutokana na urefu wa beki huyo huenda angekuwepo angefanya jambo.
Hata hivyo kelele hizo za wadau tayari zimemfikia kocha Nasredine Nabi ambaye amesema kuwa bado mapema kumchezesha beki huyo kwani anamuacha kwanza ili apate kuzoea mazingira na falsafa ya klabu hiyo.
“Nimeona watu wanaongelea sana kuhusu Mamadou (Doumbia), sio kila mchezaji akiletwa basi ataanza kucheza kwa haraka, huyu ni beki wa kati na hilo ni Eneo ambalo halihitaji kumuingiza mtu kwa haraka haraka,linahitaji utulivu ili mtu aingie”
“Huyu sio Mshambuliaji ambaye anaweza kuja na ukampa nafasi haraka haraka,hizo ni nafasi ambazo Mchezaji anaweza kuja asubuhi na jioni ukaona Uwezekano wa kumpa nafasi ya kucheza hata Kwa dakika 20”.
Doumbia amesajili kipindi cha dirisha dogo kwa lengo la kuja kuongeza uzoefu na upinzani katika eneo la kati la beki la klabu hiyo.