“Aliyekuja na jua kali, sasa anapigwa na mvua ya maswali.” Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu Kocha Mkuu wa klabu ya Simba SC, Fadlu Davids, ambaye kwa sasa yuko njia panda kati ya historia na hatima yenye mashaka.
Kocha huyo alikuja kama shujaa, mwenye mbinu mpya, macho ya scouting, na kiburi cha kutengeneza kikosi cha ndoto. Tajiri wa Simba Sc Mohamed Dewji akampa mamlaka makubwa – yaani usajili wa mastaa, benchi lake, na hata mfumo wa mazoezi ikiwemo kambi maalumu nchini Misri ambapo wengi walimuita “Fundi Mpya wa Msimbazi.” Akasajili mastaa wapya 12, wengine kutoka Afrika Kusini, DR Congo, Ghana hadi Ivory Coast – wakisifiwa kama silaha mpya dhidi ya Yanga Sc na timu za kimataifa.
Lakini baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa watani zao wa jadi Yanga SC kwenye Ngao ya Jamii, upepo umebadilika. Simba waliingia kama simba, lakini wakatoka kama paka waliozama kwenye dimbwi la lawama. Wadau, mashabiki na hata baadhi ya viongozi wakaanza kumlenga Fadlu: “Mbinu zake hazina makali, mpira wake ni kama mazoezini tu na sijui huku Misri walienda kufanya nini?,” mmoja wa mashabiki alisikika akilalama kwenye jukwaa la Benjamin Mkapa.
KUTOKA MSIMBAZI KWENDA MAGHREB?
Habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu zinasema kuwa Fadlu Davids tayari amepokea ofa ya kuvutia kutoka klabu mojawapo ya Ligi Kuu ya Morocco — mshahara unaelezwa kuwa ni mara tatu ya anayolipwa Msimbazi. Ni ofa ya kuvutia, lakini pia ni kama mlango wa kutoroka kutoka katika jiko linalowaka moto klabuni hapo huku ikionekana kuwa hafurahishwi na suala la kubebeshwa lawama yeye peke yake.
Taarifa nyingine zasema kuwa Fadlu hakutaka kuongozana na kikosi cha Simba kuelekea Botswana kwa mchezo wa kwanza wa CAF Champions League dhidi ya Gaborone United ambapo simu ya Mo Dewji ndio iliokoa na kuamua kwenda.Kwenye orodha ya wasafiri, jina lake lilikuwepo japo alitaka kugoma kusafiri. Inaelezwa tayari ameshajiandaa kuandika barua ya kujiuzulu kabla ya wiki hii kuisha.
Kama atafanya hivyo, basi Simba itabaki mikononi mwa kocha msaidizi Selemani Matola, huku uongozi ukihaha kutafuta mbadala wa haraka — lakini swali ni: atakuja lini na je, atapewa mamlaka kama ya Fadlu?
MAALIMU ALIYEKOSA REHEMA
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Fadlu aliaminiwa kama mkombozi, lakini sasa anatizamwa kama kocha mwenye mbinu za kawaida pamoja na kupewa mastaa aliowataka japo yeye inasemekana alihitaji mastaa aliowaita X-factors. Mashabiki wanajiuliza: “Ule mpira wa kasi na nguvu tuliouahidiwa uko wapi? Ni lini Simba itacheza soka la kinyama tena?” Huu ni mfano wa msemo wa Kiswahili: “Usimkabidhi kuku mweupe kwa mtu mwenye njaa – atamla bila doa.”
Fadlu alikabidhiwa kila kitu, lakini ameshindwa kufikia matarajio. Ushindi dhidi ya timu za Gormahia siku ya Simba Sc Day, pamoja na ushindi kwa baadhi ya michezo ya kirafiki si kipimo cha Simba ya Afrika. Kipimo ni Yanga, na CAF – na kwenye vipimo hivyo, mizani inamkataa kwani timu hiyo msimu uliopita ilicheza vizuri sana dhidi ya Al Masry pekee kwenye michuano ya Caf huku ikicheza kawaida sana dhidi ya Stelleboch na Rs Berkane.
KIZAZI KIPYA CHA SIMBA – KWA MATOLA?
Kwa sasa, jicho la mashabiki wa Msimbazi limeelekezwa kwa Selemani Matola ambaye atakua kocha wa muda pindi Fadlu akiondoka. Je, ataweza kuikamata timu hii yenye mastaa wa kila aina, na kuipa uhai mpya? Au ni wakati wa Simba kufanya usafi wa kiufundi kama ilivyofanya msimu wa 2020 walipomleta Sven?
Wengi wanasema ni wakati wa Simba kuachana na mfumo wa kocha mmoja kupewa mamlaka ya usajili. Taarifa za ndani zinasema hata baadhi ya viongozi wa ndani hawaridhishwi na mifumo ya Fadlu, wakidai “mpira ni mwingi, matokeo hakuna.”
MWISHO WA MBIO KWA KOCHA WA KIPENZI CHA MASHABIKI?
Fadlu alikuja kama kipenzi cha mashabiki wa Simba – walimkumbatia, walimshangilia, na walimwamini. Lakini sasa mapenzi yamegeuka kuwa karaha. Kama kweli ataondoka, ataacha nyuma jeuri ya usajili, ndoto za mashabiki, na orodha ndefu ya maswali yasiyo na majibu.